Monday, May 28, 2018

KIPA wa Liverpool, Loris Karius amesema hajalala usiku kucha baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Kipa huyo wa Ujerumani aliwakera mashabiki wake baada ya makosa mawili aliyoyafanya usiku wa jana yakiigharimu Liverpool kuchapwa mabao 3-1.
Na leo Karius ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akijutia makosa yake ya jana kwa kusema: "Sijalala kabisa hadi sasa...picha bado inajirudia kichwani kwangu tena na tena,". 
"Ninasikitika sana na ninaomba msamaha kwa wachezaji wenzangu, kwenu mashabiki, na kwa wafanyakazi wote. Nafahamu kwamba nimekosea kwa makosa mawili na kuwaangusha,". 

Loris Karius amesema hajalala tangu jana baada ya makosa aliyoyafanya kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa jana PICHA ZAIDI GONGA HAPA  
"Kama nilivyosema, natamani kurudisha nyuma wakati, lakimi haiwezekani. Ilikuwa mbaya haswa kutokana na sisi wote kufikiri tungewafunga Real Madrid na tulikuwa mchezoni mwa muda mrefu...
"Asante kwa mashabiki wetu wazuri waliokuja Kiev na kuwa nyuma yangu hata baada ya mchezo. Siichukulii kwa urahisi na kwa mara nyingine inanionyesha tulivyo familia kubwa. Asanteni na tuatejea kwa nguvu,". 
Kosa la kwanza lilikuja dakika sita baada ya mapumziko Uwanja wa NSC Olimpiki wakati Karius alipojaribu kumuanzishia mpira kwa papara beki wake wa kati, Dejan Lovren na ukambabatiza Karim Benzema mguuni na kuingia nyavuni.
La pili lilikuwa ni pale alipotunguliwa kwa shuti la mbali mtokea benchi Gareth Bale ambalo pamoja na kwamba lilielekea mikononi mwake, lakini mpira ukamponyoka na kuingia nyavuni.
Mara baada ya mchezo huo, Karius alikwenda mbele ya mashabiki waliokuwa na huzuni kubwa kuwaomba radhi  huku machozi yakimtoka. 

0 comments:

Post a Comment