Monday, May 28, 2018


PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linafungwa leo kwa mechi nane za kukamilisha msimu wa 2017- 2018 kwa timu zote 16 zikiingia viwanjani kukamilisha raundi ya 30 na mechi 240 za msimu huu, ambao tayari bingwa wake amekwishajulikana, Simba SC.
Mechi zote za kufunga pazi la Ligi Kuu msimu 2017- 2018 zitachezwa kuanzia Saa 10: 00 jioni ya leo, kasoro mchezo mmoja tu baina ya Yanga SC na Azam FC ambao utaanza Saa 2:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Mabingwa, Simba SC wapo mjini Songea tayari kumenyana na wenyeji, Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini humo, Lipuli na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba na Tanzania Prisons dhidi ya Singida United Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Yanga ilishinda 2-1 dhidi ya Azam FC mechi ya kwanza Januari 27, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

Mechi nyingine ni kati ya Ndanda FC dhidi ya Stand United Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mtibwa Sugar dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro, Njombe Mji FC dhidi ya Mwadui FC na Mbao FC dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Wakati Ligi Kuu inamalizika Jumatatu, tayari Simba SC ndiyo mabingwa wakiwa wamejikusanyia pointi 68 katika mechi 29, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 55 za mechi 29 na waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 52 za mechi 29.
Mechi kati ya Yanga na Azam FC inatarajiwa kuwa ya ushindani mkali kwa sababu ni ya kuamua mshindi wa pili wa msimu huu. Azam wanataka sare tu kumaliza nafasi ya pili, lakini Yanga wanahitaji ushindi ili kumaliza nyuma ya Simba wakibebwa na wastani wao mzuri wa mabao na pia kwa sababu walishinda mechi ya kwanza Chamazi.   
Njombe Mji FC tayari imeshuka Daraja kutokana na kuambulia pointi 22 katika mechi 29, wakati Ndanda FC yenye pointi 26 za mechi 29 na Maji Maji FC yenye pointi 24 za mechi 29 pia mojawapo itashuka pia baada ya mechi za Jumatatu.
Wakati timu mbili zitaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu Jumatatu, tayari African Lyon, KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zimekwishapanda kuelekea ligi ya msimu ujao, itakayokuwa na timu 20 ambayo ni ongezeko la timu nne.
Simba SC, zamani ikijulikana kama Sunderland msimu huu imetwaa taji la 19 baada ya awali kubeba katika miaka ya 1965, 1966 (kama Sunderland), 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004, 2007, 2009–10 na 2011–2012.
Lakini mahasimu wao, Yanga SC wanabaki kuwa mabingwa mara nyingi wa Ligi Kuu, baada ya kubeba taji mara 27 katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–2008, 2008–2009, 2010–2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
Timu nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ni Cosmopolitans 1967, Pan African 1982, Azam FC 2013-2014 zote za Dar es Salaam, Mseto SC 1975, Mtibwa Sugar 1999 na 2000 zote za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986 na Coastal Union ya Tanga 1988.

ORODHA YA MABINGWA WA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam) 
1966 : Sunderland (Dar es Salaam) 
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam) 
1968 : Yanga 
1969 : Yanga 
1970 : Yanga 
1971 : Yanga 
1972 : Simba 
1973 : Simba 
1974 : Yanga 
1975 : Mseto SC (Morogoro) 
1976 : Simba 
1977 : Simba 
1978 : Simba 
1979 : Simba 
1980 : Simba 
1981 : Yanga 
1982 : Pan African 
1983 : Yanga 
1984 : Simba 
1985 : Yanga 
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya) 
1987 : Yanga 
1988 : Coastal Union (Tanga) 
1989 : Yanga 
1990 : Simba  
1991 : Yanga 
1992 : Yanga 
1993 : Yanga 
1994 : Simba 
1995 : Simba 
1996 : Yanga 
1997 : Yanga 
1998 : Yanga 
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro) 
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)  
2001 : Simba 
2002 : Yanga 
2003 : Simba 
2004 : Simba 
2005 : Yanga 
2006 : Yanga 
2007 : Simba (Ligi Ndogo) 
2007 - 08: Yanga 
2008 - 09:  Yanga 
2009 -10: Simba SC
2010 -11: Yanga SC
2011 -12: Simba SC
2012 -13: Yanga SC
2013 -14: Azam FC
2014 -15; Yanga SC
2015 -16: Yanga SC
2016 -17: Yanga SC
2017 -18; Simba SC

0 comments:

Post a Comment