Thursday, August 16, 2018

Watu walikuwa wanasubiria kwa hamu kuona namna ambavyo Real Madrid wataikabili Atletico Madrid hii leo bila nyota wao Cristiano Ronaldo aliyetimkia Juventus ya nchini Italia.

Dakika ya kwanza tu ya mchezo watu walianza kuamini kwamba Real si lolote bila Cristiano Ronaldo pale Diego Costa alipoifungia Atletico Madrid goli la kuongoza.

Bao hili la Diego Costa lilimuingiza katika vitabu vya kumbukumbu vya UEFA Super Cup kwani ndio bao ambalo limewahi kufungwa mapema zaidi katika fainali za michuano hii.(sekunde 49).

Karim Benzema aliisawazishia Real Madrid goli dakika ya 26 na kufanya magoli 6 ya Real Madrid yaliyopita katika michuano ya Ulaya kuwekwa kambani na Benzema na Bale

Sergio Ramos aliifungia Real bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 63, lakini ilipofika dakika ya 79 ni Diego Costa tena ambaye aliufanya mchezo kumalizika dakika 90 kwa sare ya 2-2.

Katika muda wa nyongeza dakika ya 96 Saul Niguez aliungabisha krosi ya Thomas Lemar na kupiga shuti lililomshinda Keylor Navas kabla ya Koke kukandamizia msumari wa 4 na kuufanya mchezo kuisha kwa Atletico kuibuka kidedea cha mabao 4-2.

Kama haufahamu tu hii ni mara ya kwanza kwa Real Madrid kufungwa bao 4 kwenye mechi moja tangu janga kama hili liwakute mwezi November mwaka 2015 walipofungwa na Barcelona katika La Liga.

Kocha mpya wa Real Madrid Julen Lopetegui anakuwa kocha wa kwanza wa Madrid kuwahi kufungwa bao 4 katika mechi yake ya kwanza ya kimashindano tangu Michael Keeping afungwe bao kama hizo 1948.

0 comments:

Post a Comment