Tuesday, August 14, 2018


BODI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imethibitisha msimu huu Ligi Kuu haitakuwa na mdhamini Mkuu kufuatia kujitoa kwa Vodacom.
Kwa mujibu wa barua iliyotoka leo na kusainiwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura msimu ujao Ligi Kuu itakuwa na wadhamini, wawili tu ambao Azam Pay TV na benki ya KCB.
Katika barua yake, Wambura amesema kwamba Azam TV itatoa gawio la Sh. Milioni 162 kwa kila klabu kwa msimu, wakati KCB watatoa Sh. Milioni 15 tu kwa msimu wote huo.
“Malipo stahili kwa kila klabu kwa msimu huu kutokana na udhamini huo wa Ligi Kuu ni (kama ifuatavyo). Tsh 162,624,000 (Azam Pay TV) na Tsh. 15,000,000. Malipo kutoka Azam TV yatalipwa kwa awamu nne, wakati KCB Tanzania yatalipwa kwa awamu mbili,”amesema Wambura.
Vodacom wamekuwa wadhamini wakuu wa Ligi Kuu tangu mwaka 2002, wakiipokea kampuni ya Bia Tanzania (TBL) waliokuwa wakidhamini Ligi hiyo tangu mwaka 1996 kupitia bia yao ya Safari Lager.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na wachezaji wa Kagera Sugar katika msimu wa mwisho w Vodacom Ligi Kuu 

Na wote wanaondoka kwa sababu zinazofanana, TBL ilijitoa baada ya ongezeko la idadi ya timu katika Ligi Kuu bila kushirikishwa na safari hii Vodacom nao wanaondoka kwa sababu hiyo, ingawa Rais wa TFF, Wallace Karia amesema mazungumzo yanaendelea na kampuni hiyo ya simu na ana matumaini wataendelea. 
Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 inatarajiwa kuanza Agosti 22, ikitanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC), Mtibwa Sugar ambao utafanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Agosti 18.
Mechi za ufunguzi za Ligi Kuu zitachezwa Agosti 22 kati ya Ruvu Shooting na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Alliance na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Coastal Union na Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
Mechi nyingine ni kati ya Singida United na Biashara United Uwanja wa Namfua, Singida, Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba zote Saa 10:00 jioni na Simba SC na Tanzania Prisons Saa 1:00 usiku Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam. 
Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakamilishwa Agosti 23 kwa mechi kati ya JKT Ruvu na KMC Saa 8:00 mchana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Stand United na African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam na Azam FC dhidi ya Mbeya City Saa 1:00 usiku.
Wambura amesema kwamba msimu huu Ligi itaanza Agosti 22, 2018 na kufikia tamati Mei 19, mwakani (2019) ikiwa na jumla ya mechi 380 kutoka 240 msimu uliopita baada ya ongezeko la timu nne kutoka 16 za msimu uliopita.

0 comments:

Post a Comment