Na Saleh Ally, Cairo
GUMZO kubwa la hapa Misri ni kuondolewa kwa kiungo Amr Warda katika timu ya soka ya taifa ya Misri.
Inakuwa vigumu kujua ukubwa wa suala hilo kwa hapa Misri kama utakuwa nje au mbali na nchi hii.
Kuna
makundi matatu au zaidi kuhusiana na hilo, wale wanaoamini Warda
anayekipiga nchini Ugiriki ameondolewa katika timu ya taifa kwa kosa
dogo licha ya kutuhumiwa kumdhalilisha mwanamitindo Merhan Keller
kupitia mtandao wa kijamii. Wanaona lilikuwa ni jambo dogo tu.
Wapo
wanaunga mkono na kusisitiza aondolewe timu ya taifa milele lakini
wengine wanawapinga wakiamini wanawake wanatakiwa kuheshimiwa lakini
adhabu ni kubwa kwa Warda kwa kuwa ni mambo yake ya nje ya uwanja na
bado hawana imani na msichana anayemtuhumu kama kuna ukweli alimuonyesha
sehemu zake za siri kupitia mtandao wa kijamii akitaka wafanye ngono
kupitia mtandaoni. Yeye amekanusha.
Hii
imefanya hadi Mohamed Salah naye kujitokeza na kuandika katika mtandao
wa kijamii wa Twitter akisisitiza heshima kwa wanawake lakini
akizungumzia alichokifanya Warda, kinaweza kubadilika huko mbele pale
naye atakapokuwa amejifunza na kubadilika, hivyo adhabu si kwa ajili ya
kukomoa. Kama atabadilika, basi apewe nafasi tena kama uwezo unamruhusu.
Haya yanaweza kuwa ni yao, lakini kwa kiasi kikubwa yanafikirisha kwamba wachezaji wanapaswa kuwa na nidhamu kwa kiasi gani.
Nidhamu
si ile ya uwanjani pekee, kuwa kioo cha jamii ni kazi ngumu. Kuwa
mwakilishi wa taifa ni kazi ngumu na ya mateso, ndiyo maana taifa la
Misri, leo liko vitani lakini wanakubali kumuangusha askari mmoja sababu
ya kuhakikisha suala la nidhamu linapewa kipaumbele.
Nidhamu ni mwongozo wa maisha ya mwanadamu. Hata kama tajiri au una akili kiasi cha kutisha, bado kama hauna nidhamu utaanguka.
Tunaweza
kujifunza hilo kwa wenzetu kwa kuwa nidhamu ina ukubwa wake kwa maana
ya upana wa jambo lenyewe. Najaribu kuwakumbusha hilo na kuwaonyesha
jambo.
Nakumbusha
upande ule unapoambiwa wachezaji wetu hawana nidhamu hasa nje ya
uwanja, unaweza kusema haya hayahusiani na uwanjani na nidhamu si
muhimu.
Leo,
watende mambo ambayo ni tuhuma za kimtandao. Unaona hatua kali
zinachukuliwa kwa mchezaji ambaye baadaye atakuwa shujaa wa taifa hili
kutokana na ubora wake.
Kwa
Misri, wanapata hasara kwa kuwa baada ya mashindano kuanza hauruhusiwi
kuongeza mchezaji mwingine zaidi ya wale 23, maana yake watabaki na
wachezaji 22 na Warda ni muhimu sana kadiri michuano inavyosonga mbele.
Lakini kwa kuwa nidhamu ni muhimu na imepewa kipaumbele, amesukumwa nje.
Jiulize hapo nyumbani angefanya jambo kama hili mchezaji yeyote, kocha angeamua hivyo ingekuwaje?
Lazima tuiheshimu nidhamu na kuiamini kwamba ni msingi na kwa kila anayetaka kufanikiwa, lazima kuipigania na kuisimamia.
Kitu
cha pili, nimejifunza, watu kutofautiana ni suala la kawaida na kikubwa
ni kuheshimiana kwa kuwa kila mmoja atakuwa na mawazo yake. Si ikitokea
mtu ametoa maoni tofauti aonekane hana nidhamu au ni mtu mbaya.
Katika
jamii ya wapenda mpira kwetu sisi Watanzania, anayekuwa na mawazo
tofauti gumzo litakuwa “ametumwa”, hili ni jambo baya sana.
Hatuwezi
kuwa sawa kwenye kila kitu, ikitokea hivyo ujue huo ni unafiki
uliotukuka. Kupishana mawazo ni nyenzo ya maendeleo. Hapa Misri, wao
wanapishana na kujadiliana na hakuna ugomvi wa kudharauliana.
Wanakwenda
na huu mjadala wakiwa wanaamini tofauti kwa makundi, lakini mwisho
suala litapatiwa mwafaka na watu watakuwa wamejifunza.
Wakati
mwingine mtoa maoni anaweza kuwa anakosea sana lakini makosa yake
yakawashitua kukumbuka jambo jingine ambalo ni muhimu sana.
Ingawa
hakuwa sahihi, lakini mwisho anakuwa amesaidia. Hivyo kupitia hili la
Warda, tujifunze ubora na thamani ya nidhamu kwa wachezaji na mpira wetu
lakini maisha ya kawaida lakini tujifunze kuhusiana na mjadala
unavyoweza kubadili mambo badala ya upande au mtu mmoja au kundi la watu
kutaka kuonekana linajua kila kitu na halikosoleki.
Msisitizo
wangu ni kuyatathmini kwa mapana yake mambo ambayo yanatokea hapa Misri
na kujifunza kwa lengo la kuendeleza mpira wetu au jamii zetu ama
maisha kwa jumla.
Upo
msemo hapo kwetu unasema “maisha ni kujifunza”, na kweli kujifunza ni
mchakato unaoendelea katika maisha ya mtu siku zake zote duniani.
Rafiki
yangu mmoja aliwahi kusema kuwa hata siku ya kufa mtu hujifunza kwamba
“ahaa, kumbe watu ndiyo hufa hivi!” mtu anajifunza hadi kukata roho
jinsi kulivyo, kabla hujafikia hatua hiyo huwezi kujua.
Hivyo
ni lazima Watanzania tujifunze kwa wenzetu. Hapa Misri kwa sasa kuna
watu wa tamaduni tofauti kwa kuwa wamekusanyika watu kutoka nchi
mbalimbali, ni lazima kuna mengi ya kujifunza. Basi tufanye hivyo kwa
faida yetu na mpira wetu na maisha yetu pia.
Fin
AFCON 2019
Kundi A
Pld W D L Pts
1. Misri 2 2 0 0 6
2. Uganda 2 1 1 0 4
3. Zimbabwe 2 0 1 1 1
4. DR Congo 2 0 0 2 0
Juni 21, 2019
Misri 1-0 Zimbabwe 5:00 Usiku
Juni 22, 2019
DR Congo 0-2 Uganda 11:30 Jioni
Juni 26, 2019
Uganda 1-1 Zimbabwe 2:00 Usiku
Juni 26, 2019
Misri 2-0 DR Congo 5:00 Usiku
Juni 30, 2019
Uganda vs Misri 4:00 Usiku
Juni 30, 2019
Zimbabwe vs DR Congo 4:00 Usiku
0 comments:
Post a Comment