Na Saleh Ally, Cairo
UKITAKA
kumuuliza kila mmoja kuhusiana na mengi yaliyokuwa yanajitokeza ndani
ya kikosi cha timu ya soka ya taifa maarufu kama Taifa Stars wakati
ikishiriki michuano ya Afcon, utapata asilimia angalau 15 tu ya majibu
sahihi.
Kawaida
Watanzania tumefundishwa kuficha mambo na kuyazungumza taratibu kama
sehemu ya kiburudisho na wakati mwingine huenda jambo fulani kama
litawekwa wazi. Basi kuna nafasi ya kukomboa mengi ambayo yalikuwa
tatizo.
Kikosi
cha Taifa Stars kimecheza mechi tatu za makundi na kupoteza zote. Mechi
ya kwanza ilikuwa ni 2-0 dhidi ya Senegal, mechi ya pili ambayo Stars
ilionekana ina nafasi ya kufanya vizuri ikapoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya
Kenya.
Mwisho
ilikuwa dhidi ya Algeria wakachapwa mabao 3-0. Kwa mara ya kwanza,
wachezaji wa Stars, wengi wao wakaacha kuogopa na kucheza angalau mpira
uliokuwa unaeleweka. Lakini makosa mfululizo mwishoni mwa kipindi cha
kwanza, Taifa Stars ikaruhusu mabao matatu ndani ya dakika 15.
Mechi
dhidi ya Kenya, ndilo imewauma sana wengi ambao walipenda Tanzania
ishinde. Inawauma kwa kuwa waliona timu ilistahili kushinda.
Kweli
ilistahili kushinda na ilicheza soka linaloeleweka hadi kutangulia
kufunga mabao mawili, Kenya wakisawazisha. Ndani ya mechi hiyohiyo,
Tanzania ikaboronga tena na Kenya walipotanguliwa, ikawa safari imeisha.
Haya
mengi ni yale yaliyokuwa yakishuhudiwa tokea nje ya kikosi. Likiwemo
lile la taarifa la wachezaji kutaka kugoma wakidai dola 300 (Sh 687,233
)kwa siku. Lakini wachezaji wenyewe na baadhi ya viongozi walisema jambo
hilo halikuwepo hata kidogo.
Pamoja
na taarifa hizo za viongozi na baadhi ya wachezaji kulikataa, uchunguzi
wangu ukabaini lilikuwepo na baadaye nitakuelezea namna ilivyokuwa,
lilipoanzia na kwa nini lilitokea.
Wengi
tulikubali kwamba wachezaji wetu bado wana viwango vya chini kupambana
na wenzetu wanaotokea katika ligi mbalimbali kubwa. Lakini kama
kungekuwa na muunganiko sahihi bila ya matatizo niliyoyagundua, huenda
mambo yangeenda vizuri sana na hata kama ushindi mmoja au sare ingeweza
kupatikana.
Kocha
Emmanuel Amunike kwa muonekano ni mtu anayetia huruma sana. Kuna kila
sababu ya kumheshimu kwa kuwa anaingia katika historia ya Tanzania
kushiriki Afcon kwa mara ya pili ikiwa ni baada ya miaja 39, lakini
uhalisia amekuwa tatizo kubwa na amechangia kwa kiasi kikubwa Stars
kushindwa kufanya vema.
Niliamua
kufanya uchunguzi ili nipate uhakika wa mengi ambayo nimeona yamekuwa
athari na kama yatabaki siri, basi hakutakuwa na faida katika Afcon
nyingine tukifanikiwa kwenda.
Uchunguzi
nilioufanya kwa kina kupitia watu zaidi ya 12 wakiwemo walio ndani ya
Stars, TFF lakini hata wale ambao waliishi na timu jijini Cairo.
Kinachoshangaza
ni kila kitu kutaka kufanywa siri kwa kuwa tu kuna hofu ya siasa ambayo
imeingia ndani ya kikosi cha Stars kwa hiyo kila ambalo TFF wanaona
wanaweza kusema kwa ajili ya kurekebisha, wanaona kama siasa zitaingia
na kuleta mfarakano.
Kuna
wanasiasa walianza kulumbana sababu ya timu hiyo ambayo wengi wao
hawakuwa na msaada wowote. Lakini baadaye wengine wakaomba wapewe posho,
waliponyimwa wakaishambulia timu. Hili nalo ni siri na hakuna
anayejaribu kulisema kwa hofu ya kushikiliwa, kufikishwa mahakamani au
kulalamikiwa mitandaoni.
Uchunguzi
wangu umepita kwenye yote haya lakini leo ninaanza na Kocha Amunike
ambaye kwa kiasi kikubwa naona ndiye alikuwa adui mkubwa wa Taifa Stars
nikitoa asilimia 30 huenda hakuwa akijua kama anakosea na ninaweka
asilimia 70, alikuwa anajua analolifanya.
Wakati
wa mapumziko kwenye mechi ya Kenya, Amunike aliingia vyumbani, wengi
wakitarajia kwa kuwa Taifa Stars ilikuwa inaongoza, angetoa maelekezo
mazuri kuhusiana na kikosi nini cha kufanya kwenda kuongeza mabao na
ikiwezekana kuwazuia kabisa Wakenya.
Muda wote wa mapumziko katika vyumba vya Taifa Stars kwenye Uwanja wa 30 June ulitumika kwa malumbano ya kupita kiasi.
Kelele za wachezaji wakionyesha kukasirishwa na kile alichokisema kocha baada ya kumtukana beki Kelvin Yondani.
Moja
ya tusi alilolitoa Amunike kwa Yondani ni kumuambia anacheza kama
mwanamke. Kitu kilichowashangaza wengi kwa kuwa waliamini Yondani
alipambana sana siku hiyo.
Kitendo
hicho cha Amunike kutoa matusi na kebehi kwa wachezaji wake, tena beki
aliyekuwa akionekana kuwa tatizo kwa washambuliaji wa Kenya,
kiliwashitua wachezaji wengine wakataka kujaribu kuhoji, Amunike akawa
mkali sana huku akisema maneno makali.
Kutokana
na hali hiyo, Yondani akaanza kububujikwa machozi ikionekana dalili
zote kwamba angeshindwa hata kucheza kipindi cha pili.
Baadhi
ya wachezaji walianza kumbembeleza Yondani aliyekuwa amejiinamia kwa
takribani dakika moja na nusu akilia kimyakimya huku akifuta machozi.
Nahodha Mbwana Samatta akaamua kuchukua jukumu hilo kama nahodha kwa kuzungumza tofauti na namna alivyokuwa amezungumza Amunike.
ENDELEA KUSOMA KESHO JUMAMOSI katika blogu hii ya SALEHJEMBE. USIKOSE.
MECHI ZA TAIFA STARS AFCON:
Vs Senegal 2-0
Vs Kenya 3-2
Vs Algeria 3-0
0 comments:
Post a Comment