Friday, September 13, 2019


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta atakosekana kesho klabu yake, KRC Genk ikimenyana na wenyeji, Sporting Charleroi kuanzia Saa 3:30 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji usiku Uwanja wa Pays de Charleroi.
Hiyo ni kutokana na maumivu madogo yanayomsumbua kwa sasa, kufuatia kuumia akiichezea Tanzania dhidi ya Burundi katika mchezo wa kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Akizungumza na blog hii leo kwa simu kutoka Ubelgiji, Samatta amesema kwamba Daktari amemshauri kupumzika kwa siku chache baada ya kuumia mwishoni mwa wiki.

Mbwana Samatta (kulia) akiwa na mchezaji mwenzake wa Taifa Stars baada ya mechi na Burundi 

“Aliniambia si maumivu mabwa, japo ilibaki kidogo yawe makubwa, sehemu ya mguu ndiyo inaonekana kushtuka, lakini haijakatika, pia sehemu ya ndani ya mguu imeachia, ndiyo maana ina maumivu, kwa hiyo nitulize mguu siku chache utakaa sawa,”amesema Samatta.
Nahodha huyo wa Taifa Stars aliondoka uwanja wa dakika ya 106 baada ya kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, kiungo Himid Mao Mkami ‘Ninja’ anayechezea ENPPI ya Misri ambaye alikwenda kuiongoza timu kumalizia mechi vizuri ikiitoa Burundi kwa penalti 3-0 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Mapema Samatta aliitanguliza Taifa Stars kwa bao lake la dakika ya 30 akimalizia kona ya beki wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy anayechezea Nkana FC ya Zambia, kabla ya Abdulrazak Fiston kuisawazishia Burundi dakika ya 45 akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji chipukizi, Amissi Mohammed.
Mchezo huo ukamalizika kwa sare ya 1-1 na kufanya sare ya jumla ya 2-2 kufuatia sare nyingine ya 1-1 mjini Bujumbura Jumatano iliyopita na Tanzania ikaenda kushinda kwapenalti 3-0 jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Beki mkongwe anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni alianzisha biashara nzuri kwa Taifa Stars baada ya kufunga penalti ya kwanza na wenzake, kiungo Himid Mao Mkami ‘Ninja’ na beki Gardiel Michael Mbaga wakafunga pia.
Kaseja aliwakata maini Warundi baada ya kuokoa penalti ya kwanza ya Int’hamba Murugamba iliyopigwa na mtokea benchi, Gael Duhayindavyi aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kanakimana Bienvenu Kanakimana dakika ya 67 na haikuwa ajabu Saido Berahino na Bigirmana Gael wakapiga nje mfululizo.

0 comments:

Post a Comment