GUMZO la jijini Mwanza ni ujio wa Yanga na uamuzi wa timu hiyo kucheza mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga itakuwa jijini hapa kwa zaidi ya wiki moja kuanzia jana Jumamosi kwa vile watacheza mechi ya Ligi dhidi ya Mbao FC Jumanne hii kisha Jumapili na Pyramids ya Misri.
Pitapita ya Spoti Xtra kwenye vijiwe mbalimbali vya mikoa ya Kanda ya Ziwa imebaini kwamba amshaamsha na hamasa ya mashabiki imekuwa juu sana hususani kwenye matawi makubwa ya Yanga ya Shinyanga na Mwanza.
Hata kabla timu hiyo haijawasili jana asubuhi, mashabiki walikuwa wakihamasishana kununua jezi pamoja na kwenda kwa wingi uwanjani kwenye mechi ya Jumanne ambayo wamedai ndiyo itakayotoa uelekeo wa Jumapili.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera baada ya kuwasili na kikosi hicho jana alisisitiza kwamba sasa ni mwendo wa mazoezi bandika bandua mpaka kieleweke.
Alisema kwamba wachezaji waliokuwa kwenye timu ya Taifa watakuwa wamewasili kufikia leo na programu ya kwanza ni kumaliza mechi ya Mbao halafu waunganishe na ile ya Waarabu.
Alisisitiza kwamba mazingira ya Mwanza ni mazuri na wamefurahi sapoti kubwa wanayopata kutoka kwa wanachama na mashabiki.
Yanga jana walipiga tizi mchana kwenye Uwanja wa Chuo cha Butimba na leo wataendelea kama kawaida. Timu hiyo imekuwa ikikusanya kijiji na kushangiliwa kila basi lao linapoonekana kwenye mitaa ya Mwanza.
Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kila kitu kipo sawa na kwa hali anavyoiona Wanayanga watafurahi kwani mazuri yanakuja mbele yao.
0 comments:
Post a Comment