Monday, October 21, 2019


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia amefunguka juu ya taarifa za kutangazwa kwa kocha mpya wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ atakayechukua nafasi ya Etienne Ndayiragije ambaye alikuwa hapo kwa muda.

Kupitia mahojiano yake na kipindi kipya cha michezo cha Sports Arena kilichoanza kurushwa leo na Wasafi FM chini ya Mtangazaji Maulid Kitenge na Edo Kumwembe, Rais Karia amesema mpaka sasa TFF imeshapokea barua za maombi ya kazi pamoja na simu kutoka kwa makocha mbalimbali duniani.
”Kusema kweli tunamshukuru Mwenyezi mungu, ametuwezesha tumeweza kufuzu kwenda CHAN kama ambavyo tulivyozungumza na kocha Etienne Ndayiragije kwamba tunamuomba kwaajili ya kutuvusha kwakuwa mabadiliko yalitokea mapema tu kabla ya wiki mbili kabla ya kuanza CHAN, Emmanuel Amuneke akawa ameondoka.” Amesema Rais Wallace Karia.
Rais Karia ameongeza ”Kwahiyo tulimuambia kwamba jukumu lake tunalompatia ni kutuvusha, kashatuvusha tunamshukuru M/Mungu kwa sasa tunasubiri ripoti yake ambayo ataiwasilisha leo Shirikisho TFF. Pia tunasubiri Technico Committe iwakilishe ripoti yake.”
”Tuna barua za maombi ya kazi za makocha ‘Application Letter’ zaidi 200 kutoka duniani huko na wengine wanapiga simu kila siku.”
”Kwa hiyo kwa vigezo vizuri kabisa, hali halisi ya Tanzania na mazingira ya wachezaji wetu lakini pia na mashindano ambayo yapo mbele yetu kwasababu mwezi ujao tunacheza na Libya pamoja na Equatorial Guinea kwaajili ya  qualification ya AFCON 2021.”
”Kwa hiyo muda si mrefu, hata wiki hii haita kwisha tutawatangazia kocha ambaye atakuwa amependekezwa na kamati ile ya ufundi lakini pia na kupitishwa na kamati ya utendaji.”
Rais Wallace Karia amemaliza kwa kusema ”Sio kwamba kocha Etienne Ndayiragije ameondoka Azam basi ndiyo anakuja TFF hapana, lakini asipigiwe debe wapo wanaofanya shughuli hiyo.”
Etienne alikaimu nafasi hiyo baada ya kufukuzwa kwa kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kufuatia Taifa Stars kupoteza mechi zote tatu za Kundi C kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019.

0 comments:

Post a Comment