Thursday, October 10, 2019



Mshambuliaji Kylian Mbappe ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, kinachoendelea na maandalizi ya michezo ya kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2020), dhidi ya Iceland na Uturuki.

Taarifa zilizotolewa na shirikisho la soka nchini Ufaransa (FFF) zimeeleza kuwa, mshambuliaji huyo aliondoka jana kambini, na kurejea kwenye klabu yake ya PSG kwa ajili ya kuanza matibabu.

Mbappe, alipatwa na majeraha ya paja akiwa katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya juma lililopita dhidi ya Borussia Moenchengladbach ya Ujerumani, na iliaminiwa hakuumia sana na ndio maana aliitwa kwenye timu ya taifa ya Ufaransa.

Hata hivyo hali ya mshambuliaji huyo haikuridhisha alipofika kambini mwanzoni mwa juma hili, na ameshauriwa kurejea jijini Paris, kufanyiwa matibabu ya jeraha lake.

Ufaransa wataanza kukipiga dhidi ya Iceland ugenini kesho ijumaa katika mchezo wa kundi H, na kisha watarejea nyumbani kuwakabili Uturuki katika mpambano unaotarajiwa kuwa na vuta nikuvute siku ya jumatatu.

Mabingwa hao wa dunia wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi H wakiwa na alama 15, nyuma ya Uturuki ambao katika mchezo wa kwanza uliopigwa mjini Konya mwezi Juni, waliwabanjua Ufaransa.

Iceland wanakamata nafasi ya tatu katika kundi hilo, kwa kufikisha alama 12 zilizotokana na michezo sita waliyocheza mpaka sasa.

0 comments:

Post a Comment