Friday, October 4, 2019


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana ameisaidia timu yake KRC Genk kupata pointi ya kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya sare ya bila kufungana na Napoli ya Italia katika mchezo wa Kundi E usiku wa jana Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk. 
Samatta aliyekuwa Nahodha wa Genk kwa mara nyingine jana, alikuwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki wazoefu wa Napoli, Mreno Mario Rui, Giovanni Di Lorenzo na Msenegali, Kalidou Koulibaly ambaye klabu hiyo ya Italia ilikataa dau la Pauni Miloni 91 kumuuza Manchester United miezi miwili iliyopita.
Hata hivyo, Samatta aliyewahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Anayecheza Afrika kabla ya kuhamia Ulaya, alifanikiwa mara kadhaa kuwatoka mabeki hao na kukaribia kufunga katika mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa.

Beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly (kushoto) akiwa juu kuokoa dhidi ya mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta 

Wakati Genk inaokota pointi ya kwanza kwenye michuano hiyo baada ya mechi mbili, Napoli inafikisha pointi nne na kuendelea kuongoza Kundi E kufuatia jana Liverpool kushinda 4-3 dhidi ya Salzburg ya Austria ambazo zote sasa kila moja ina pointi tatu.
Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26 jana amecheza mechi yake ya pili tu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa amefunga bao moja kwenye mchezo uliopita wakifungwa 6-2 na Salzburg ya Austria.

Mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta akimtoka beki wa Napoli, Mreno Mario Rui jana

Kwa ujumla, Samatta amecheza mechi 166 kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.
Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 130 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 na mabao 14. 
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Coucke, Mæhle, Cuesta, Lucumi, Uronen, Berge, Hrosovsky, Hagi, Ito, Bongonda/Paintsil dk90 na Samatta.
Napoli; Meret, Di Lorenzo, Manolas, Koulibaly, Mario Rui/Malcuit dk34, Elmas/Mertens dk58, Ruiz, Allan, Lozano, Milik/Llorente dk72 na Callejon.

0 comments:

Post a Comment