MPIRA wa Tanzania kwa sasa tunazungumzia mambo mengi sana ya msingi ili kuhakikisha tunatoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi.
Tayari
tunajua faida ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kufikia hatua ya
robo fainali kama ambavyo walifanya Simba kabla ya kufeli msimu huu.
Hivyo
kama itakuwa Simba, Yanga, Azam FC au timu nyingine itafanikiwa zaidi
ni furaha ya changamoto ambayo inatuongoza kufanya mambo mengi sana kwa
weledi.
Lazima
tupige hatua lakini si kazi nyepesi, kuna mambo mengi sana ya kufanya
kama kukuza vijana kwa misingi sahihi, kuendeleza soka la watoto,
wanawake na kufanya mpira uwe biashara badala ya furaha ya moyo pekee.
Ndio
maana utaona hata katika klabu, sasa hata wale waliokuwa na ngozi ya
chuma kupinga uwekezaji sababu ya ushabiki tu wa moyo au sababu ya
maslahi yao binafsi, sasa wameanza kubadilika na kukubaliana.
Kama
haya ni malengo ya Tanzania kwa ujumla, vipi leo klabu mbili kubwa kama
Yanga na Azam FC ziko katika mgogoro mdogo kabisa usiokuwa na sababu za
msingi.
Nazungumzia
kuhusiana na mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Ditram Nchimbi
aliyekuwa Polisi Tanzania kwa mkopo na sasa amesajiliwa na Yanga.
Taarifa tulizonazo, Yanga na Azam FC wamemalizana na tayari wanaamini
mchezaji huyo atahamia Yanga.
Kiutaratibu,
ili aingizwe kwenye mfumo na kuweza kucheza ligi kuu, Azam FC lazima
wakubaliane na Polisi Tanzania na mkataba huo uingizwe kwenye mfumo wa
wachezaji wa TMS ambao unamruhusu mchezaji kutambulika na Bodi ya Ligi
ya yuko timu gani.
Wakati
anapelekwa Polisi kwa mkopo, maana lazima hao Polisi watoe fedha kidogo
kama walivyosema na wameeleza kuwa mkopo wao na makubaliano yao na
Nchimbi ni mwaka mmoja. Sasa haujaisha, kama anataka kuhama lazima kuwe
na makubaliano tena kati yake, Azam FC, Nchimbi na hao Polisi.
Ukweli,
Yanga wanaweza kuwa wamefuata utaratibu sahihi kwa kuwafuata wamiliki
sahihi ambazo ni Azam FC. Lakini wanaingia kwenye ugumu kwa Nchimbi
hajamalizana na Polisi ambao bila shaka wataleta ugumu mwishoni.
Katika
hali ya kawaida unajiuliza, kama mpira wetu kwa sasa hesabu ni kufika
mbali, vipi kuwe na malumbano ya aina hii katika kipindi hiki. Faida
yake ni nini hasa?
Kama
tunajadili mambo mengi ya msingi, vipi huyu mchezaji anayekwenda timu
nyingine baada ya timu yake kukubali kumuuza, imeshindwa vipi
kukubaliana na timu ambayo walikubaliana kumchukua kwa mkopo hadi suala
hili litambae hewani na kuwa ishu kubwa wakati kuna mengi sana ya msingi
ya kufanya kwenda katika maendeleo ya mpira wetu.
Binafsi
naona ni mambo yaliyopitwa na wakati na tukubaliane, vyovyote
mnavyofikiri, Nchimbi anapaswa kukubali kuwa Polisi Tanzania wamekuwa na
msaada mkubwa kwake kuonekana hata kuliko Azam FC hivyo anapaswa
kuwaheshimu wakati anaondoka.
Tunapaswa
kujifunza suala la uungwana hata kama utakuwa unaondoka sehemu moja
kwenda nyingine. Thamani ya pale ulipokuwepo, ndiyo iliyokutengenezea
kile ambacho wengine wanakiona.
Polisi
Tanzania walitoa nafasi kwa Nchimbi kucheza, akaweza kuifunga Yanga hat
trick, ikavutiwa naye. Yes ni mchezaji wa Azam FC, sasa vipi leo
aondoke na kushindwa kumalizana na Polisi Tanzania eti hadi wafikie
hatua ya kufungua kesi au “kufa” naye kama walivyosema wao.
Tujifunze
kwenye kila tatizo, timu hazipaswi kuingia hofu ya kuwachukua wachezaji
kwa mambo kama yanayoendelea. Wala wachezaji hawapaswi kuzidharau timu
zilizowachukua kwa mkopo hata kama wamiliki wao wamemalizana na
wanunuzi.
Kweli
Polisi walikuwa na mpango na Nchimbi, makubaliano ni mwaka mmoja,
akiondoka kabla, tofauti na makubaliano ni kuwaingiza kwenye mipango
mipya ambayo haikuwepo. Basi waheshimuni na Azam FC, Nchimbi katikati na
Polisi Tanzania mkae meza moja na mmalize suala hili dogo lisilo na
nafasi zama hizi za kufikiria mambo mengi ya msingi kwenda katika
mabadiliko.
0 comments:
Post a Comment