LIVERPOOL
ilishika nafasi ya pili katika Ligi Kuu England, nafasi ya pili katika
Ligi ya mabingwa Ulaya wakati kocha mkuu akiwa ni Jurgen Klopp.
Klopp
huyo raia wa Ujerumani, bado ni kocha mkuu wa Liverpool. Kwa sasa ndiye
ameiwezesha kubeba mataji matatu makubwa ndani ya mwaka mmoja.
Liverpool
hawataisahau 2019 kwa muda mrefu sana, wamekuwa mabingwa wa Ulaya,
wamebeba ubingwa wa Super Cup ya Ulaya na sasa ni mabingwa wa dunia kwa
klabu, wakifanikiwa kuishinda Flamengo ya Brazil.
Wakati
wakiishinda Tottenham katika fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya, hakuna
ubishi, Liverpool walionekana kweli walikwenda kucheza fainali wakiwa
watu ambao walijifunza kupitia makosa yao ya fainali ya mara ya mwisho
dhidi ya wababe Real Madrid ambao wakati wanakutana na Liverpool ilikuwa
ni fainali yao ya tatu mfululizo na wakafanikiwa kubeba ubingwa kwa
mara ya tatu mfululizo na kuandika rekodi mpya na ngumu kuivunja katika
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati
wanakutana na mabingwa wa Europa League, Chelsea, hakuna aliyekuwa na
uhakika, lakini uchezaji wao haukuwa ule wa fainali ya Ligi ya Mabingwa
Ulaya.
Walicheza
tofauti kwa aina iliyoonekana wazi walitambua wanacheza na mabingwa wa
upande mwingine wa Ulaya. Wakaibuka wababe na kuchukua Super Cup.
Kwa
Kombe la Dunia, timu za England haziwezi kuwa na kelele nyingi sana, si
michuano zinayofanikiwa kufika mara nyingi au kubeba kombe hilo mara
kwa mara. Ni Manchester United pekee walikuwa wamelitwaa mwaka 2008
chini ya Alex Ferguson.
Mara
ya mwisho, Liverpool walicheza fainali ya michuano hiyo mwaka 2005,
wakakutana na Sao Paulo ya Brazil na kukubali kipigo cha bao 1-0, kombe
likapelekwa Brazil.
Mwaka
2012, Chelsea nao wakaingia fainali, wakakutana na kipigo cha bao 1-0
kutoka Corinthias ya Brazil, kombe likaenda Brazil tena.
Kuanzia
2012, hakuna timu ya England iliyokuwa imegusa fainali ya michuano
hiyo. Ikawa hivi; mabingwa wa Ulaya ni Bayern Munich, fainali dhidi ya
Raja Casablanca (2013), mabingwa Real Madrid, fainali dhidi ya San
Lorenzo (2014), bingwa FC Barcelona, fainali dhidi ya River Plate
(2015), bingwa Real Madrid dhidi ya Kashima (2016), Madrid tena dhidi ya
Gremio (2016), Madrid tena dhidi ya Al Ain (2018).
Mwaka
2019 umekuwa ni wa England na waliopeleka kombe ni Liverpool ambao
wamefuta uteja wa timu za England dhidi ya zile za Brazil katika fainali
ya Kombe la Dunia. Hakuna ubishi tena kuwa Kocha Klopp ni ufunguo mpya
ambao umerudisha faraja na kutengeneza mwamko mpya ambao haukutegemewa.
Utaona
jambo moja, wakati mwaka 2015 Klopp akitua Liverpool akitokea Borussia
Dortmund, deni kubwa kwake lilikuwa ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu
England ambao Liverpool kwao umekuwa ni kama “ugonjwa usio na tiba”.
Zaidi
ya miaka 29 wamekuwa wakiusikia, lakini wamekuwa na mashabiki wenye
roho ngumu zaidi ile ya paka, kwani wamebaki na kumbukumbu ya historia
ambayo wengine hata hawakuwa wamezaliwa au kujitambua vizuri. Lakini
wakaendelea kujivunia bila ya woga.
Walichotaka
ni kubeba ni ubingwa wa England lakini Klopp anaonekana kutokana na
namna walivyotaka Liverpool, yeye ameanza tofauti kabisa. Badala ya
kuanzia chini kwenda juu, anatokea juu kurejea chini.
Ana
ubingwa dunia, Super Cup ya Ulaya, ubingwa wa Ulaya na sasa anashuka
kwenda kwenye ubingwa wa England ambao kiuhalisia hadi sasa inaonekana
vigumu sana kuwazuia.
Kwa
wanavyokwenda kama hakutakuwa na mabadiliko, suala la ubingwa kwao ni
la kusubiri kwa kuwa wazi wanaonekana hawako tayari tena kufanya makosa
ya msimu mmoja au miwili iliyopita na hilo wamalithibitisha kwa kubeba
makombe matatu ndani ya mwaka mmoja.
Kikosi
cha Liverpool, msimu uliopita kiliteleza mwanzoni na mwisho kikashindwa
kuendana na kasi ya Manchester City. Safari hii, Klopp ameonyesha
Liverpool hii si ile ya msimu uliopita, wanajua wanataka nini kwa wakati
gani na mambo yanafanyika kwa wakati mwafaka.
Liverpool
wanacheza kulingana na wanachotaka, wanashinda kutokana na wanayekutana
naye. Bado hawajapoteza hata mchezo mmoja katika EPL ndani ya mechi 18
na wanaongoza kwa tofauti ya pointi 10 na anayeishika nafasi ya pili
Leicester City, tena wakiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya yake.
Uchezaji
wao unaonyesha wazi, Liverpool hawakuchanganywa na kuukosa ubingwa wa
Ulaya, kuukosa ubingwa wa EPL mwishoni lakini wakatumia muda wao
kujifunza wapi walipokosea na Klopp amekuwa ufunguo wa Liverpool ya
zamani yenye mambo ya kisasa na hakuna kinachoshindikana mbele yao kwa
sasa kwa kuwa Klopp ni ufunguo mpya unaotumika kufungua mlango imara wa
zamani.
0 comments:
Post a Comment