Monday, December 30, 2019






MUNICH, Ujerumani
LIGI Kuu ya Ujerumani maarufu kwa jina la Bundesliga kwa sasa ipo katika mapumziko mafupi kupisha kipindi cha Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.


Ligi hiyo ambayo huwa inarushwa ‘live’ na StarTimes, ni ligi pendwa katika mataifa mengi duniani, inasifika kwa kuchezwa soka la nguvu.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka huu 2019 kuna maoni yametolewa kuhusu ligi hiyo, ambapo yalikusanywa maoni ya mashabiki kuhusu kikosi bora kwa muda wa miaka 10 iliyopita.


Maoni hayo yalihusisha wachezaji wote waliocheza hapo kati kwenye ligi hiyo kuanzia mwaka 2010 hadi sasa ambapo zimesalia siku kadhaa tu kumalizika kwa mwaka 2019.


Hiki hapa ni kikosi bora kwa mujibu wa maoni ya mashabiki ambayo waliyatoa kupitia mitandao ya kijamii huku asilimia kubwa wachezaji wametoka katika timu mbili Bayern na Dortmund;


Kipa
Manuel Neuer
Timu: Schalke na Bayern 
Mwanzoni Neuer alikuwa chaguo la kwanza la Schalke na kuiwezesha kubeba taji la German Cup mwala 2011. Baadaye akawa bora zaidi alipotua Bayern na hata katika timu ya Taifa ya Ujerumani.


Ameshinda mataji saba ya Bundesliga, manne ya ndani ya Ujerumani, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia. Staili yake ya kuwa kipa kama beki ilichangia kuleta mapinduzi ya jinsi makipa walivyotakiwa kucheza.


Beki wa kulia
Philipp Lahm
Timu: Bayern 
Beki ambaye alikuwa tegemeo katika kikosi cha Bayern na Ujerumani kwa miaka mingi, alidumu katika ubora wa juu kabla ya kuanza kupotezwa na kocha Pep Guardiola ambaye badaye alimbadili majukumu na kumfanya kuwa kiungo.

Ajabu ni kuwa huko nako alifunika na kuwa katika ubora wa juu, hali ambayo ilimfanya kupata sifa nyingi kutoka kwa Guardiola. Alistaafu soka mwaka 2017.

Beki wa kati
Mats Hummels
Timu: Dortmund, Bayern 
Alianza kufanya kweli Dortmund baadaye akawavutia Bayern walioamua kumbeba.
Kuna kipindi alikuwa mmoja wa mabeki bora wa kati duniani na kuzivutia klabu nyingi kuwa. Anasifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo.

Beki wa kati
Jerome Boateng
Timu: Bayern Munich
Baada ya kutofanikiwa akiwa Manchester City alihamia Bayern ambapo huko akawa tegemeo na kujitengenezea uimara wa kuwa beki kisiki. Uwezo mkubwa wa kutumia nguvu ulimsaidia kuwadhibiti wapinzani wengi.

Beki wa kushoto
David Alaba
Timu: Bayern 
Alianza kuonekana kwenye Bundesliga, Februari, 2010, akimtengenezea bao Franck Ribery. Tangu hapo akawa anatumika kama beki na kiungo. Akiwa na umri wa miaka 27 tu tayari ameshacheza mechi 232 za Bundesliga.


Kiungo mkabaji
Bastian Schweinsteiger
Timu: Bayern 
Injini muhimu ya Bayern iliyochangia mataji matatu mwaka 2013, pamoja na ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka mmoja baadaye. Aliitumia nusu ya miaka yote hapo kati kuichezea Bayern kabla ya kwenda Manchester United kisha Chicago Fire. 


Ameshastaafu kwa sasa lakini bado mchango wake unakumbukwa na wengi hasa Wajerumani.


Kiungo wa kati
Ilkay Gündogan
Timu: Dortmund
Kiungo mchezeshaji ambaye kwa sasa yupo Man City ya England lakini miaka ya nyuma akiwa chini ya kocha Jürgen Klopp waliifanya Dortmund kubeba mataji mawili mwaka 2012.

Gündogan alisajiliwa akitoka Nuremberg mwaka 2011, hakucheza muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi 


Kiungo mchezeshaji
Marco Reus
Timu: Gladbach, Dortmund
Mtu pekee katika orodha hii ambaye hajabeba taji lakini bado sifa yake ni kubwa kutoka na uwezo binafsi ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani. 

Kwa sasa ni injini ya Dortmund, ni mzuri katika kuichezesha timu japokuwa amekuwa akisumbuliwa na majeraha.


Winga wa kulia
Arjen Robben
Timu: Bayern 
Alistaafu Julai, 2019 lakini hiyo haijazuia jina lake kupotea, aliwafanya kitu kibaya walinzi wengi wa Bundesliga.

Mholanzi huyu alikuwa hatari kwa kasi yake uwanjani hasa alipokuwa akiutumia mguu wake wa kushoto.


Winga wa kushoto
Franck Ribery
Timu: Bayern 
Patna wa muda mrefu wa Robben, ushirikiano wao ulikuwa hatari na walicheza kwa kuelewana muda mwingi, Mfaransa huyu alidumu klabuni hapo kwa miaka 12.

Mkali wa kukokota mpira aliyekuwa Mchezaji Bora wa Ulaya wakati Bayern ikibeba mataji matatu mwaka 2013. Bado anacheza akiwa na umri wa miaka 36, yupo Italia akiitumikia Fiorentina.


Straika
Robert Lewandowski
Timu: Dortmund, Bayern
Straika mwenye uwezo mkubwa wa kufunga, umbo lake kubwa na mwenye akili ya kiwango cha juu katika kuwasoma walinzi.

Amecheza mechi 305 na kufunga mabao 220 kiasi kwamba ana wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 110, akiwa na mataji saba. 


Kocha 
Jürgen Klopp
Timu: Dortmund

Sasa hivi anaitawala dunia akiwa Liverpool, lakini enzi zake akiwa Dortmund aliiwezesha kupata mataji mfululizo mwaka 2011 na  2012. Hakushinda mataji mengi lakini bado sifa zake zimewazidi Pep Guardiola na Jupp Heynckes walipata kura nyingi pia katika maoni hayo.

0 comments:

Post a Comment