KOCHA
wa timu ya Yanga, Charles Mkwasa amesema ushindi walioupata kwenye
mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons umewapa nguvu
ya kujipanga kuikabili Biashara United katika mchezo utakaochezwa kesho
kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Mkwasa
alitoa kauli hiyo juzi baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi kwa
kuifunga Tanzania Prisons bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja
wa Samora Iringa, na kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi
wakiwa na pointi 21.
Alisema
wanauchukulia mchezo huo kama fainali kwa kuwa ni moja ya timu
zinazoonesha ushindani mkubwa kutafuta matokeo hususani kwenye viwanja
vya ugenini.
“Ninawashukuru
wachezaji kwa ushindi tuliopata kwani umetuongezea nguvu ya kujipanga
kwenye mchezo wetu unaokuja dhidi ya Biashara United kuhakikisha
tunapata matokeo kama haya kujipanga na mchezo wetu wa Januari 4 dhidi
ya Simba,” alisema Mkwasa
Alisema
mchezo uliopita walicheza kwa kiwango cha juu kwa kumiliki mpira na
kutengeneza nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza lakini wachezaji
wake walikosa umakini na kushindwa kumalizia kupata mabao ambayo
yangewafanya kumaliza mchezo kipindi cha Kwanza.
Alisema
kipindi cha pili wapinzani wao walicheza mpira wa nguvu na kupiga
vikumbo kuwatoa mchezoni jambo ambalo walifanikiwa lakini alitoa
maelekezo kwa wachezaji wake kurudi nyuma kulinda ushindi waliopata
kipindi cha kwanza.
Naye
kocha wa Tanzania Prisons, Mohamed Rishaard ‘Adolf’ alikubali matokeo
na kukiri kufanya makosa katika dakika za mwanzo na kufungwa bao jambo
ambalo hakulitegemea.
“Sina
sababu ya kusema uwanja shida lakini kimsingi tulifanya makosa na
kuruhusu kufungwa bao la kizamani jambo ambalo sikutegemea, nimekubali
kama benchi la ufundi tunaenda kujipanga na ratiba ya mechi zinazokuja
kuhakikisha tunapata ushindi” alisema Adolf Alisema matokeo hayo kwa
kiasi fulani yamevuruga malengo yao kwani ilikuwa ni kulinda rekodi yao
ya bila kufungwa lakini kukosa umakini dakika za mwanzo zimewafanya
wafungwe.
0 comments:
Post a Comment