Licha
ya kupanda katika viwango vya dunia, matokeo ya bondia wa ngumi za
kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo na Arnel Tinampay raia wa Ufilipino
yameshindwa kuwekwa kwenye mtandao wa Boxrec kutokana na kutokidhi
vigezo vilivyowekwa.
Mwakinyo
alimshinda Tinampay kwa pointi katika pambano la raundi kumi, uzito wa
super welter ambalo halikuwa la ubingwa lililofanyika Novemba 29, mwaka
huu kwenye Uwanja wa Uhuru.
Boxrec
ni mtandao ambao unahusika kuhifadhi rekodi na matokeo za mabondia wote
duniani ambao unamilikiwa na John Sheppard raia wa Uingereza lakini
hadi kufikia jana Jumanne ulikuwa haujaonyesha matokeo ya pambano hilo.
Mwakinyo
alisema kuwa kwa upande wake hadi sasa hajui kitu gani kinapelekea
matokeo yake yanashindwa kuwekwa kwenye mtandao huo licha ya kupewa
maneno mengi ambayo hajui mwisho wake.
“Kiukweli
hadi sasa sijui nini tatizo ambalo limepekelea matokeo yangu kuchelewa
kuwekwa Boxrec maana nimekuwa nikiambiwa maneno mengi kwa sababu wapo
wanaosema kwamba kuna bondia wa Tanga alicheza siku ile hakuwa na kibali
hivyo ni ngumu kuweka hadi kipatikane.
“Lakini
niliongea na rais wa kamati ya ngumi, yeye alisema imeshindikana
kupokelewa kwa kuwa hakutuma video za ushahidi Boxrec hivyo hawatoweza
kuingiza matokeo hadi zipatikane kwani wao hawakuweka mtu wa kuchukua
tukio hivyo lazima waende Azam kwani hata kupanda kwenye viwango kufikia
nafasi ya 17 kati ya mabondia 1858 duniani imetokana na rekodi za
nyuma,” alisema Mwakinyo.
Championi
lilimtafuta rais wa kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBCR), Joe
Anea kwa njia ya simu lakini hakuweza kupokea simu licha ya kuita muda
mrefu na hata alivyotafutwa katibu wake, Yahaya Poli naye hakuweza
kupokea simu.

0 comments:
Post a Comment