Tuesday, December 31, 2019


Kiungo wa Barcelona, Arturo Vidal, amechukua hatua ya kushangaza dhidi ya klabu yake hiyo. Ameamua kuishtaki akidai hajalipwa pauni milioni 2 (Sh bilioni 6) za bonasi mbalimbali.

Wanasheria wake wa Chile walipeleka mashtaka mahakamani Desemba 5 wakidai nyota huyo mwenye umri wa miaka 32, alitakiwa kupewa bonasi mbalimbali baada ya msimu wake wa kwanza Barcelona kufuatia kutua akitokea Bayern Munich.

Vidal aliichezea Barcelona mechi 53 msimu uliopita waliposhinda ubingwa wa La Liga na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wanasheria wa Vidal wanasema anatakiwa alipwe bonasi ya pauni milioni 2 kwa kucheza asilimia 60 ya mechi hizo za Barca.

Lakini taarifa ya gazeti la Hispania la ABC, inasema madai yake hayo yanapingwa vikali na Barcelona ambao wanadai hakufikisha angalau dakika 45 kwa mechi. Wanadai wanasheria wake wametafsiri vibaya vipengele katika mkataba wake.

Vidal anaamini alikuwa anadai pauni 3,500,637 lakini alipewa pauni 1,446,388 tu.

0 comments:

Post a Comment