Monday, December 30, 2019



IMEISHA hiyo! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya beki wa kati wa Simba, Muivory Coast, Pascal Wawa, kudai kwamba, ameziangalia vizuri mbinu za mshambuliaji wa Yanga, David Molinga, ni mzuri ‘jembe’, lakini anaamini hatoweza kumsumbua wakikutana.

Wawa ametoa kauli hiyo kuelekea katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga unaotarajiwa kuchezwa Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Simba ambayo juzi Jumamosi ilicheza dhidi ya KMC, kabla ya mchezo huo ilikuwa inaongoza ligi ikiwa na pointi 28 kutokana na kucheza mechi 11, huku Yanga ikishika nafasi ya tatu ikijikusanyia pointi 20 katika mechi kumi ilizocheza.

“Nimejipanga vizuri kwa kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huo, nimeangalia safu yao ya ushambuliaji ikiongozwa na Molinga, kiukweli haipo vibaya.

“Unajua yule siyo mchezaji mbaya kama watu wengi wanavyomchukulia, ukiangalia alivyoanza kucheza na sasa amekuwa tofauti, hivyo nafahamu nini cha kufanya ili asitupe wakati mgumu kutokana na ubora wake ingawa hawezi kunisumbua,” alisema Wawa.

0 comments:

Post a Comment