Monday, January 13, 2020



Golikipa wa Azam FC, Razak Abalora amesema anaamini siku zote kuwa yeye ni mshindi licha ya kukosa penalti ya mwisho kwenye mchezo wa juzi, huku kipa wa Simba Beno Kakolanya akisema alishajiwekea uhakika kwenye penalti tano, lazima aokoe mbili au moja.

Makipa hao timu zao zilikutana juzi katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Amaan Zanzibar, ambapo Simba ilifuzu fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa penalti 3-2 baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.

Akizungumza Abalora alisema anaamini yeye ni mshindi, licha ya kukosa penalti ya mwisho na kuifanya timu yake kuachia kombe, kwani ilikuwa bingwa wa msimu uliopita.

“Nilikosa penalti lakini naamini mimi ni mshindi kwenye mchezo ule, kwani nilipangua penalti mbili pia,” alisema Abalora.

Naye Kakolanya ambaye aliibuka shujaa kwa kufuta penalti ya golikipa mwenzake wa Azam FC alisema alijiwekea malengo ya kupangua mbili au moja na akafanikiwa.

“Nilishajiwekea uhakika,kwenye penalti tano, lazima niokoe mbili au moja,” alisema Kakolanya ambaye alifanikiwa kupangua penalti moja ya kipa wa Azam FC wa kuipatia Simba ushindi.

Katika mchezo huo ambao ulianza saa 2:15 juzi penalti za Simba zilifungwa na Erasto Nyoni, John Bocco na Jonas Mkude na Azam FC zilifungwa na Yakubu Mohamed na Bruce Kangwa.

Waliokosa kwa Simba ni Sharaf Shiboub na kwa Azam FC walikosa ni Idd Kipagwile, Donald Ngoma na Razak Abalora. Simba fainali inakutana na Mtibwa Sugar, ambayo iliiondoa Yanga kwa penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya 1-1, ambao unatarajiwa kuchezwa kesho.

0 comments:

Post a Comment