SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) limeiagiza Kamati ya Maadili kufuatilia ukweli
kuhusu tuhuma za upangaji wa matokeo zilizotolewa na kipa wa Yanga,
Ramadhani Kabwili.
Akizungumza
Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema baada ya
TFF kusikia tuhuma hizo zilizotolewa na Kabwili kupitia vyombo vya
habari, sekretarieti imeiandikia barua Kamati yake ya Maadili kufanyia
kazi suala hilo.
“TFF itavijulisha vyombo vingine vya usalama ili visaidie uchunguzi na kuchukua hatua stahiki,” alisema Ndimbo.
Kabwili
ambaye ni kipa wa tatu Yanga, amenukuliwa na kituo kimoja cha redio
nchini akiishutumu Simba kutaka kumpa hongo kwa ajili ya kufanikisha
mpango wa kupanga matokeo.
Alidai
Simba ilimshawishi afanye kosa kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania
litakalomfanya aoneshwe kadi ya njano na kufikisha idadi ya kadi
zitakazomsababisha akose mechi iliyofuata dhidi ya watani wa jadi katika
soka ya Tanzania.
Hata
hivyo, Kabwili aliyesimama langoni kwenye mechi dhidi ya Simba Februari
16, mwaka jana, Yanga ikifungwa 1-0, bao pekee la mshambuliaji Meddie
Kagere dakika ya 72 alisema hakukubali kushiriki mpango huo.
Wakati
mchezaji huyo akisubiri kwenda kwenye Kamati ya Maadili ya TFF, Klabu
ya Simba imepinga na kukemea vikali kauli ya Kabwili.
Katika
mtandao wao wa Instagram jana, Simba walisema wanapinga vikali kauli
hiyo aliyoitoa juzi katika kituo cha Redio cha East Afrika, na
kusisitiza kwamba inaamini kauli za aina hii kutoka kwa wachezaji ni za
kuchukiza na sio za heshima ambazo zinaashiria upangaji wa matokeo ya
mechi kama ilivyotuhumiwa na mchezaji huyo.
Ilisema:
“Kauli hizi zina madhara makubwa kwenye uadilifu wa klabu ya Simba na
uongozi wake, heshima kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania inawekwa
mashakani kama kauli za namna hii hazitachukuliwa hatua stahiki”.
Taarifa hiyo ilisema Simba inafurahishwa na hatua za haraka
zilizochukuliwa na TFF dhidi ya kauli kama hizi kwa vyombo husika.
“Simba
inaamini jambo hili lipo mbele ya mikono ya vyombo husika na
litachukuliwa hatua stahiki haraka,” sehemu ya taarifa hiyo ilisisitiza.
0 comments:
Post a Comment