NAHODHA
wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ni mchezaji halali wa Aston Villa
inayoshiriki Ligi Kuu England na tayari ameanza kazi kwenye kikosi
hicho.
Aston
Villa hivi sasa inajiandaa kucheza dhidi ya Manchester City katika
mchezo wa Fainali wa Kombe la Carabao, na jumamosi itacheza mchezo wa
Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth.
Ni
hatua kubwa imepigwa na Samatta katika maisha yake ya soka kwani
ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo ambayo
wachezaji wengi duniani wamekuwa wakiwa na ndoto ya kucheza hapo.
Samatta
alikuwa na ndoto ya kucheza hapo, ndoto zake zimetimia na sasa jukumu
lililobaki ni kuweka rekodi zaidi na zaidi ikiwemo kucheza timu kubwa
zaidi ya Aston Villa.
Haikuwa
kazi nyepesi ya kulala na kuamka kisha Samatta kutua Aston Villa,
alijitoa, akapambana kufanikisha hili ambalo limetokea kwa sasa.
Kufika
hapo kwa Samatta, ni deni kwa wachezaji wengine wa Kitanzania nao
kufuata nyayo zake ili kuwa na namba kubwa ya wachezaji wetu wakicheza
ligi kubwa Ulaya.
Ya
Samatta yamepita, lakini yabaki vichwani mwa Watanzania wengi hasa
wachezaji soka kwamba na wao wana deni, wanapaswa kulilipa.
Katika
hatua nyingine, tumeona makundi yamepangwa ya mechi za kufuzu Kombe la
Dunia michuano inayotarajiwa kufanyika Qatar mwaka 2022.
Tanzania
imepangwa Kundi J na timu za DR Congo, Benin na Madagascar. Ukiangilia
kwa haraka unaweza kusema ni kundi jepesi, lakini ni gumu hasa kwetu.
Mwaka
jana tulishiriki Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) kule Misri, na timu
tulizopangwa nazo zenyewe zilishiriki michuano hiyo ambapo sisi
tuliishia hatua ya makundi tukishika nafasi ya mwisho.
Kundi
letu katika Afcon tulikuwa chini ya Senegal, Algeria na Kenya,
hatukuweza kushinda hata mchezo mmoja. Kwa ufupi, tulifanya vibaya.
DR
Congo, Benin na Madagascar zilifanya vizuri zaidi yetu. DR Congo
iliishia 16 bora, Madagascar wakafika robo fainali kama ilivyo kwa
Benin.
Madagascar
ambao waliingia Afcon kama timu isiyopewa nafasi, iliiondosha DR Congo
na kuingia robo fainali, huko ikakutana na Tunisia, safari yao ikaishia
hapo.
Benin wao robo fainali walifungwa na Senegal, timu ambayo tulicheza nayo hatua ya makundi na kutufunga.
Kocha
wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, anapaswa kulitambua hili kwamba,
Watanzania wanahitaji kuiona timu ikifanya vizuri na ikiwezekana
inakwenda Qatar kushiriki michuano hiyo.
Hatuwezi
kufika Qatar kama hatutakuwa na mipango madhubuti, lazima tukubali tupo
kwenye kundi gumu, tukikubali tumepangwa kundi jepesi, itakuwa hatari
zaidi kwetu.
Kukubali
kwamba sisi ndiyo timu ya kiwango cha chini kwenye kundi hilo
haimaanishi kwamba hatuwezi kupambana, hiyo itawafanya wachezaji
kupambana zaidi, matokeo yake tutafikia malengo.
Dua na sala za Watanzania hivi sasa ni kuona tunashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Tukiwa tumeshiriki Afcon mara mbili, basi tuna deni la kushiriki Kombe la Dunia. Mikakati iwekwe kufikia malengo hayo.
0 comments:
Post a Comment