Mwaka 2019 ulikuwa na mengi yalitokea na hatimaye ukurasa umefungwa na taratibu tumeanza kuumega mwaka 2020 ni suala la kushukuru kwa Mungu na kuomba atujalie uzima wakati mwingine tuonane tena mwaka ujao.
Basi yote tunayoyapanga tusisahau kwamba hapa tunapita na kazi yetu kubwa kwa sasa ni kuishi kwa amani na upendo hakuna namna nyingine ya kufanya zaidi ya hayo tu ndugu yangu.
Leo napenda kuzungumzia juu ya mchezo ambao umezidi kuwa juu kwa wadau na wafuatiliaji wa soka Bongo na nje ya Bongo ni kutokana na msisimko wake ambao upo kwenye soka.
Itakuwa ni mechi ya kwanza ndani ya mwaka 2020 ambayo itakuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kubwa zinazosaka ubingwa wa ligi kuu.
Simba ni mabingwa watetezi walitwaa msimu uliopita na sasa wanaingia kwenye vita kupambana na Yanga ambao walianza kwa kusuasua kabla ya kurejea kwenye mstari na sasa vita imepamba moto.
Itakuwa ni Januari 4, 2020 ni siku ambayo mchezo huu unatarajiwa kuchezwa uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 wakitazama uhondo ndani ya uwanja huo.
Kikubwa ni kuona kwamba kila mmoja anatafuta ushindi utakaowafanya wawe ndani ya vita ya kufuata ulipo ubingwa ila kikubwa tunachohitaji ni burudani safi na sio vita kwa mashabiki na wachezaji.
Ukweli ni kwamba nchi itasimama kwa muda kushuhudia watani wa jadi wakipiga mechi yao ya kwanza ya msimu wa 19/20 kitu ambacho kinasubiriwa kwa shauku kubwa.
Ni mechi ambayo imebeba hisia kubwa kwa pande zote za Yanga/ Simba mchezo huu huwa hautabiriki kirahisi kwa wapinzani wote wawili kutokana na kila timu kujiandaa kwa presha kubwa na hofu.
Huwa haitabiliki kwenye matokeo yake bila kujali ni timu ipi ipo vizuri kiuchumi ama ipo vibaya kiuchumi haina hiyo ni vita ya kweli ambayo haichagui silaha ila ikikupata inakupoteza jumla.
Kila timu imekuwa na mbinu zake ambapo kwa upande wa Simba imekuwa ikitegemea sana viungo katika kuandaa mashambulizi na kumalizia jambo ambalo linaifanya iwe na unyumbulifu muda mwingi.
Mkwasa naye ana mbinu yake ya kushambulia kwa kushtukiza na kutumia mabeki wake kuanzisha mashambulizi huku viungo wake wakiwa nao kwenye ubora wake jambo linaloongeza utamu.
Matumaini yangu kwamba, Charlse Mkwasa anajua vema mbinu za mpinzani wake na Sven Vanderbroeck naye anatambua mbinu ya mpinzani wake jambo litakalonogesha vita ya watani hawa wa jadi.
Kitu cha msingi ni kwa kila timu kujiandaa vema na kufanya maandalizi mazuri nje na ndani ya uwanja ili waweze kupata matokeo ambayo wanahitaji kuyapata ndani ya uwanja.
Marefa watakaopewa jukumu la kuchezesha mechi hiyo wanapaswa wafuate sheria 17 za mpira ili kuongeza ile ladha ya soka ndani ya uwanja bila kutibua mambo.
Nina amini kwamba endapo kila mmoja atatimiza jukumu lake kwa wakati tutampata mshindi kwa haki bila vurugu zozote zile na mtindo wa kuvunja viti utasahaulika milele.
Mshindi ni yule ambaye atajiandaa vema na sio yule atakaywekwenda na matokeo uwanjani huyo amejiandaa kufeli mapema kabla ya mchezo.
0 comments:
Post a Comment