MZAZI
wa mshambuliaji wa Aston Villa ya nchini Uingereza, Mbwana Samatta,
Mzee Ally Samatta, amemtaka kijana wake huyo abadili mwenendo katika
klabu yake hiyo mpya ili kuhakikisha anakuwa bora zaidi ya alivyokuwa
KRC Genk ya Ubelgiji alikotokea.
Samatta
amesajiliwa katika Klabu ya Aston Villa hivi karibuni, akitokea Genk
kwa dau la pauni milioni 8.5 huku akijiwekea rekodi ya kuwa Mtanzania wa
kwanza kujiunga na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya England.
Aidha
nahodha huyo wa Taifa Stars tayari ameshaichezea timu yake hiyo mechi
mbili, ikiwa ni dhidi ya Leicester katika nusu fainali ya Carabao Cup
ndani ya dakika 65 huku akishindwa kufumania nyavu licha ya kukosa bao
moja la wazi.
Pia,
juzi Jumamosi, Samatta alifumga bao lake la kwanza tangu ajiunge na
timu hiyo, pia likiwa ni bao pekee kwa Aston Villa ambao hata hivyo
walishindwa kutamba ugenini mbele ya Bournemouth ambao waliibuka na
ushindi wa bao 2-1.
Mzee
Samatta alifunguka kuwa, kama mzazi amejisikia vyema kuona mtoto wake
huyo anakipiga katika ligi kubwa duniani lakini amemtaka aongeze juhudi
zaidi ya alivyokuwa mwanzo.
“Nimefurahi
kuona mwanangu anakuwa Mtanzania wa kwanza kuchezea ligi kubwa duniani,
kwani mzazi yeyote amekuwa akipenda kuona mwanawe anafikia mafanikio.
“Kitu
ambacho nimemtaka akifanye kwa sasa ni kuhakikisha anaongeza juhudi
mara mbili zaidi ya ile aliyokuwa akiifanya Genk kwa kuwa ligi hiyo ni
kubwa na ina ushindani zaidi, hivyo ajipange kuhakikisha anakuwa katika
kiwango bora,” alisema mzee Samatta.

0 comments:
Post a Comment