IMEELEZWA kuwa uongozi wa Yanga uwamewalipa wachezaji wake mishahara ya miezi miwili sambamba na bonasi zao za mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Hiyo yote ni katika kuelekea mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la FA utakaowakutanisha na watani wa jadi, Simba Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa, Yanga wataingia uwanjani wakihitaji rekodi na ushindi ili wavuke hatua ya fainali na kulichukua kombe hilo ili wafuzu kucheza mashindano ya kimataifa, wakati Simba wenyewe wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi.
Habari zinaeleza kuwa wachezaji hao walilipwa mishahara na bonasi hizo saa chache mara baada ya kuanza safari ya kuelekea Musoma kwenda kucheza na Biashara United.
Mchezo huo ulikamilika kwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Karume.
Chanzo hicho kilisema kuwa, lengo la kulipa madai hayo ya wachezaji ni kuwaongezea morali ya kucheza kwa bidii ili wafanikishe ushindi katika mchezo huo wa FA.
“Hakuna mchezaji yeyote anayedai mshahara na bonasi za mechi za ligi na FA, viongozi wameona umuhimu wa mchezo wa nusu fainali watakaokutana na Simba na ndiyo sababu ya kuwalipa mishahara, bonasi wachezaji wetu.
“Sasa hivi wachezaji ndiyo tunawadai wao, kwa kuhakikisha wanafanikisha ushindi katika michezo tuliyoibakiza ukiwemo huu wa ligi dhidi ya Biashara kabla ya kumalizia na Kagera Sugar.
“Uongozi unauchukulia umuhimu mkubwa mchezo huo wa FA tutakapocheza dhidi ya Simba, hivyo tumekamilisha malipo yao ya mishahara na bonasi, pia uongozi hivi sasa unaandaa kambi nzuri ya timu katika kuelekea mchezo wa watani wetu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuzungumzia hilo, alisema: “Sisi tumeandaa utaratibu mzuri wa malipo ya mishahara ya wachezaji, hivyo katika timu yetu hakuna mchezaji anayedai mshahara wala posho.
0 comments:
Post a Comment