Thursday, October 1, 2020



BEKI wa Yanga, Lamine Moro, amefunguka kuwa kama kiungo wa timu hiyo, Carlos Carlinhos, raia wa Angola ataendelea kupata nafasi ya kucheza, basi yeye atakuwa anafunga sana kwa kuwa ni mtu ambaye anamjulia.

Lamine Moro amefunga mabao mawili, ndani ya dakika 270 alizocheza ambazo ni sawa na michezo mitatu kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

 

Alifunga bao pekee kwa Yanga kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar kisha akafanya hivyo pale Jamhuri dhidi ya Mtibwa na mabao yote ni ya kona zilizochongwa na Carlinhos.

 

Lamine amesema, Carlinhos ni mchezaji mzuri sana kwenye mipira ya kona na faulo, lakini jambo zuri zaidi anafahamu namna ya kupiga mipira ambayo inaipa faida timu, hivyo kama mchezaji huyo atadumu kwenye kikosi cha Yanga basi atakuwa anafunga sana.


“Carlinhos Mungu amempa kipaji kikubwa cha kucheza mipira iliyokufa, anajua kuchonga kona na kupiga faulo nzuri na zenye malengo. Kama ataendelea kuwa vile, mimi naweza kusema nitafunga sana msimu huu,” amesema Lamine.


Yanga ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Oktoba 3,Uwanja wa Mkapa ambao ni wa raundi ya tano.


Kwenye msimamo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi 4 ikishinda 3 na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Mkapa,kinara ni Azam FC mwenye pointi 12 ambaye ameshinda mechi zote nne kwa msimu wa 2020/21.

 

0 comments:

Post a Comment