MZUNGUKO wa nne wa Ligi Kuu Bara umekamika kwa michezo tisa kupigwa kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini ambapo, wapo ambao wameendelea kuvuna pointi tatu muhimu, waliotoa sare na kugawana pointi lakini.
Pia wapo wale ambao kwenye mechi zao mambo kwao bado sio mazuri baada ya kushuhudia wakipoteza michezo mbele ya wapinzani wao kwenye ligi.
Niliwahi kusema hapo kabla kuwa msimu huu utakuwa mgumu hasa kutokana na ubora wa vikosi vyote ambavyo vimepata nafasi ya kushiriki, nadhani hivi sasa kwa kutazama matokeo ya michezo iliyopigwa na namna ambavyo msimamo wa ligi unaonekana kila mtu anaweza kuwa shahidi wa kile nilichowahi kukisema.
Ushindani huu ambao niliwahi kuutabiri ni miongoni mwa vitu ambavyo naamini huko mbeleni vitatusaidia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa viwango vya wachezaji na timu zetu kiujumla na kutufanya tuweze kufanya vizuri pale tunapokwenda kucheza dhidi ya timu ambazo ziko mbele katika nyanja ya soka barani Afrika na Dunia kiujumla.
Jambo la muhimu kwa wachezaji wetu hasa katika hali kama hii ya ushindani ni kuhakikisha wanakuwa na nidhamu kuanzia nje na ndani ya uwanja ili huo ushindani unaoendelea kuonekana miongoni mwa vikosi vya timu mbalimbali uwe wa faida na burudani na sio kuugeuza kuwa matukio ya uhasama.
Katika kudumisha hali ya amani viwanjani na kuitikia kauli mbiu inayotolewa na shirikisho la soka duniani FIFA wa 'fair play' yaani mchezo wa kiungwana, mashabiki wanaoingia viwanjani na hata wale wanaofuatilia matangazo ya televisheni wanapaswa kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa hili.
Hivi karibuni yaliripotiwa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani yaliyotokea viwanjani ambapo wahusika wakuu wa matukio hayo wakiwa ni mashabiki, mfano wa matukio hayo ni lile la mashabiki kutaka kumshambulia mwamuzi wa mchezo wa Mbeya City dhidi ya Azam kutokana na kile walichokieleza kuwa ni upendeleo.
Hali hiyo ilipelekea vurugu kubwa kiasi cha kulazimisha Polisi waingilie kati na kumtoa mwamuzi huyo pamoja na maofisa wa mchezo huo uwanjani kupitia gari la Polisi.
Nakubali kuwa mpira ni mchezo wa hisia na kila mtu ana chaguo la timu anayoipenda na kutamani kuona inafanikiwa hasa kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umekuwa ukifanyika lakini sio vizuri tukawa watumwa wa hisia kiasi cha kuhatarisha maisha yetu au ya wale wanaotuzunguka bali mpira utufanye kuzidi kudumisha umoja, urafiki na mshikamano wetu.
Jambo jingine ambalo nadhani ni muhimu tukakumbushana ni hili la maandalizi ya kutosha kwa timu zote kuelekea kwenye michezo iliyo mbele yao ambalo kwa kiasi kikubwa linawahusu viongozi wa timu, kutokana na ugumu ambao unazidi kuonekana ndani ya ligi ya msimu huu ni vyema viongozi wa timu zote wakaziandaa vya kutosha timu zao.
Kwanini nasema hivi, unapokuwa umeandaa timu yako vizuri unakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya msingi dhidi ya waamuzi au hata kuepukana na matukio yasiyokuwa ya kimichezo ambayo kiukweli yanatia aibu.
Mfano mzuri ni tukio lililofanywa na mojawapo ya timu za ligi kukataa kuingia uwanjani kupitia maeneo rasmi ya kuingilia uwanjani na kulazimika kuchana nyavu tukio lililohusishwa na imani za kishirikina.
Ukiachana na fedheha ambayo timu inaipata kutokana na matukio ya namna hii lakini pia yanaakisi kutokujiamini kwenye suala la maandalizi hivyo kupelekea hofu zisizo na msingi hivyo ni muhimu kwa viongozi wa timu na mabenchi ya ufundi yakaandaa timu zao vya kutosha.
Miongoni mwa vitu vilivyonifurahisha msimu huu ni kuona nyota wengi ambao walikuwa na kiwango kizuri msimu uliopita wakianza vyema msimu huu, wachezaji kama Reliants Lusajo, Yusuph Mhilu, Jaffary Kibaya wote wanaonekana kuwa bora lakini pia yapo maingizo mapya ya wachezaji waliosajiliwa ambao wameanza kufanya vizuri.
Kuna msemo wa Waswahili usemao biashara asubuhi jioni mahesabu nadhani ndio neno ambalo ningependa kuwaambia nyota wetu hawa ili wajue kuwa wana wajibu wa kujituma zaidi wakati huu kabla ligi haijachanganya na kuwa ngumu zaidi huko mwishoni.
Kwa kila mchezaji mwenye malengo yake ndani ya msimu huu anapaswa kujua muda wa kuyatimiza ni sasa asisubiri wakati ujao atakwama.
Napenda kuchukua nafasi hii pia kuupongeza Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jitihada mbalimbali ambazo wamekuwa wakizionyesha katika suala la usimamizi wa ligi ikiwemo hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa hivi karibuni kwa kuvifungia viwanja ambavyo vimeonekana kuwa na mapungufu mbalimbali hasa eneo la kuchezea.
Ni wazi kuwa kama tunataka maendeleo kwenye mpira wa miguu hapa nchini lazima tuhakikishe tunaboresha miundombinu ya viwanja ikiwemo; eneo la kuchezea, vyumba vya kubadilishia nguo, majukwaa, vyoo na kadhalika lakini nadhani lingekuwa jambo la busara zaidi kama ukaguzi na fungiafungia hii ya viwanja ingefanyika kabla ya msimu kuanza ili kuepusha usumbufu na gharama za kuzihamisha timu kutoka sehemu moja kwenda nyingine katikati ya msimu.
Pia katika hili la kufungia viwanja linafikirisha kwa kuwa kawaida ni kwamba kabla ya mchezo ukaguzi huwa unafanyika hata kabla ya ligi kuanza ukaguzi huwa unafanyika bado sijajua msimu huu mambo
yalikuajekuaje.
0 comments:
Post a Comment