Thursday, November 26, 2020


VIGOGO, Yanga SC wamepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Azam FC leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Shujaa wa Yanga SC ni leo ni kiungo wake, Deus Kaseke aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 48 akimchamba kwa mguu wa kulia kutoka umbali wa mita 14 kipa David Mapigano Kissu kufuatia pasi maridadi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacpouba Sogne. 
Refa Emmanuel Mwandemba aliyesaidiwa na Charles Simon na Kassim Mpanga aliwaonyesha kadi za njano mabeki Mghana Lamine Moro wa Yanga SC, Mganda Nico Wadada na mshambuliaji Muivory Coast, Richard Ella D’jodi wa Azam FC kwa makosa tofauti.
Na kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 28 na kupanda kileleni, ikiwazidi pointi tatu Azam FC baada ya timu zote kucheza mechi 12 – wakiwa mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 23 za mechi 11.


0 comments:

Post a Comment