Thursday, November 26, 2020

 



KIPA wa zamani wa timu ya Taifa ya England Peter Shilton ambaye alikuwa langoni kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kati ya England dhidi ya timu ya Taifa ya Argentina amesema kuwa Diego Maradona hakuwaomba msamaha wachezaji wote baada ya kuwafunga bao la mkono.

Maradona ambaye ni gwiji na Legendi kwenye maisha ya mpira amefariki jana Novemba 25 kutokana na mshutuko wa moyo ikiwa ni mwezi mmoja tangu atimize miaka 60 na Rais wa Taifa la Argentina Alberto Fernandez ametangaza siku tatu za maombelezo kwa ajili ya kuheshimu mchango wa nyota huyo kwenye masuala ya mpira na kulitangaza taifa lao.

Kwenye mchezo huo wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia, Maradona alifunga bao kwa mkono ambapo mwamuzi hakuweza kuliona na kulikubali jambo lililowapa nafasi Argentina kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 na iliweza kutwaa taji la Kombe la Dunia mwaka 1986.


Akiwa nahodha Maradona alicheza mechi zote mwaka huo na alifunga mabao matano na kutoa jumla ya pasi tatu, jumla kwenye timu ya Taifa ya Argentina tangu mwaka 1977-1994 amecheza mechi 91 na kuifungia timu hiyo mabao 34.

Kipa huyo amesema kuwa licha ya timu yao ya Taifa ya England kuwa na wachezaji wazuri hawakuwa na namna ya kumzuia Maradona kutokana na uwezo wake kwa kuwa alikuwa ni hatari kuliko wachezaji wengine wote ndani ya kikosi.


"Hakukuwa na mpango maalumu wa kumdhibiti kwa kuwa alikuwa ameshindikana ndani ya uwanja, uwezo wake mkubwa na akili nyingi, hakuna ambaye aliweza kumzuia licha ya kwamba na sisi tulikuwa na kikosi imara na tuliamini kwamba tungeweza kutinga hatua ya fainali.

"Sisi sote tulijua nini ambacho kingetokea baadaye sasa tungefanya nini kwa mfano? Alinipa changamoto kwenye mpira wa juu, alidanganya kwamba amepiga kichwa na alijua kwamba angeshindwa kuupata kwa kichwa, alichokifanya ni kuupiga kwa mkono ili ujae ndani ya nyavu na hicho ndicho kilichotokea.


"Ulikuwa ni udanganyifu wa wazi kabisa aliufanya na alikuwa anajua kwamba hakuwa na chaguo la kufanya kwa kuwa alifanya hivyo alikimbia haraka na kuanza kushangilia kwa nguvu, alimtazama refa mara mbili huku akisubiri maamuzi yake yatakuaje. 

"Mbali na mwamuzi wa kati pia walikuwepo waamuzi wa pembeni alijua kwamba alichokifanya sio sawa ila hakuwa na chaguo, tulikuwa na huzuni kubwa sana baada ya mpira kuisha ndani ya chumba cha kubadilishia nguo ila tungefanya nini?

"Kwa kile alichokifanya hapana, hakuweza kuomba msamaha hata mara moja kwa kusema kuwa alifanya udanganyifu hapana,sehemu yoyote ile hajawahi kusema kwamba alidanganya zaidi amekuwa akitumia neno 'Mkono wa Mungu' katika hili sio sawa.

"Bobby Robson, aliyekuwa Kocha Mkuu alikuja na kutuuliza alishika kwa mkono?  Akatikisa kichwa ila ni kwamba baada ya mchezo ule hakuweza kutuomba msamaha wachezaji wote na kila tulipokuwa tukikutana alikuwa akizungumza habari nyingine kabisa," amesema.


Pumzika kwa amani Maradona.

0 comments:

Post a Comment