ISRAEL Mwenda, nyota mpya ndani ya kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes amefanikiwa kuweza kuuteka ufalme wa Mohamed Hussein, “Tshabalala’ kwa muda kwenye mechi yake ya kwanza ya ushindani ndani ya ligi.
Mwenda aliibuka ndani ya Simba akitokea KMC ambapo ujio wake ulikuwa unatajwa kukutana na ushindani mkubwa ndani ya Simba kutokana na uwepo wa mabeki wengine, Shomari Kapombe na Tshabalala.
Akiwa na jezi ya Simba, katika mchezo wa kwanza wa ligi mbele ya Biashara United aliweza kuanza moja kwa moja kikosi cha kwanza na kutumia dakika 90 kuonyesha kile ambacho kimejificha kwenye miguu yake.
Kipindi cha kwanza alicheza namba tatu huku Kapombe akiwa ni namba mbili na dakika zote hizo aliweza kuwa mwiba kwa Biashara United ambapo aliweza kufanya majaribio manne na yote yaligota kwenye mikono ya kipa wa Biashara United, James Ssetupa.
Kipindi cha pili Tshabala alivyoingia akitokea benchi alibadili upande ambapo Tshabalala alicheza namba tatu, Mwenda namba mbili napo aliendelea kuwa mwiba kwa kutimza majukumu yake vizuri.
Mzawa huyo ameweza kuutikisa ufalme kwa muda wa Tshabalala na Kapombe hivyo ana deni la kupambana zaidi kuwa bora kwani kazi bado ipo na mechi za ushindani ni nyingi.
Simba ni mabingwa watetezi ambapo mchezo wao wa kwanza walianza kwa kulazimisha sare hivyo wana kazi kwenye mchezo wao wa pili dhidi ya Dodoma Jiji unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri,Dodoma.
Aliyofanya Mwenda ilikuwa ngumu kufanywa na nyota wengine wa Simba ikiwa ni pamoja na David Kameta ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo ndani ya Biashara United mwingine ni Gadiel Michael ambaye bado yupo ndani ya Simba.
Pia Mwenda jina lake limetajwa kwenye orodha ya wachezaji walioitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars hivyo anajukumu la kulinda ubora wake kwa kuwa ni hazina ya Tanzania.
0 comments:
Post a Comment