DAKTARI Dhamana Wilaya ya Mjini Ramadhan Mikidadi Sleiman, amewataka wanamichezo na jamii kiujumla kujitokeza kwa wingi kupatiwa chanjo ya uviko (Covid 19) ambayo inapatikana bure katika vituo vya afya 44 kwa Zanzibar nzima.
Akiyasema hayo huko Uwanja wa Amaan Studium wakati wa zoezi la kupatiwa chanjo ya Covid 19 ya (Johnson Johnson) kwa wanamiichezo mbali mbali wa Zanzibar .
Amesema matarajio ni kuchanja wanamichezo 65 hadi 70, hata hivyo idadi inaweza kuongezeka na kuwahakikishia wanamichezo hao, chanjo hizo ni salama haina madhara imethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Alifahamisha kuwa, mtu ambae amepatiwa chanjo ya covid 19 iwapo atapata maradhi hayo madhara huwa ni madogo sana, vilevile chanjo hiyo inauwezo mkubwa wa kupunguza vifo kutokana na ugonjwa huu wa korona .
Alibainisha kuwa, katika Wilaya ya Mjini, vituo ambavyo vinatoa chanjo ya covid 19 ni Vituo cha afya Rahaleo na Mpendae na hivi karibuni wanatarajia kutoa huduma hiyo katika vituo vya Kwamtipura pamoja na Polisi Ziwani.
Nae Afisa Afya ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto, Yahya Mselem Mbwana amesema hadi sasa zaidi ya watu elfu 20 wameshapatiwa chanjo hizo .
Alifahamisha kuwa muitikio wa watu sio mbaya lakini bado uhamasishaji unahitajika kutokana na Idadi ya watu waliojitokeza bado ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu waliopo .
Amesema kuwa iwapo kutajitokeza Taasisi za Serikali na binafsi ambao inawafanyakazi wengi wanahitaji huduma ya chanjo wawapatie taarifa na idadi iliopo watawafuata popote walipo kuwapatia huduma ya chanjo hiyo .
Afisa huyo alitoa wito kwa jamii kuwataka wajitokeze kwa wingi katika chanjo hiyo hasa yale makundi maalum ikiwemo wazee ,wafanyakazi katika sekta ya utalii, wanafunzi, walimu wahudumu sekta ya afya pamoja na wanaofanya kazi sekta ya usafiri ikiwemo Bandarini na Uwanja wa Ndege.
Kwa Upande wa Katibu wa Kamati ya Soka la Wanawake, Dhuwaiba Aboud Mikidadi amesema njia moja wapo ya kujikinga maradhi ya covid 19 ni kupata chanjo kwa kulinda afya hivyo, amewataka wana jamii waondokane na hofu kwani chanjo ni salama haina madhara yoyote imethibitishwa na wataalamu wa afya .
Meneja wa Timu ya Taifa Zanzibar Hashim Salum Hashim amewataka wanamichezo kuitikia wito wa kupatiwa Chanjo ya Covid 19 ili kujinusuru na maradhi hayo kutokana na kuwa kinga ni bora kuliko tiba .
0 comments:
Post a Comment