Tuesday, November 21, 2017


MECHI za wikiendi hii za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinazozihusu Simba na Yanga zitachezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
Hiyo inafuatia Uwanja wa Uhuru kuwa na matumizi mengine ya kijamii na wakati huo huo, Uwanja wa Taifa bado haujaruhusiwa kwa matumizi kufuatia ukarabati wa eneo la kuchezea.
Yanga watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya Jumamosi wakati Simba wataikaribisha Lipuli ya Iringa Jumapili katika mfululizo wa Ligi Kuu mjini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga watahamia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi

Taarifa ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata kutoka Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema kwamba kwa sababu hiyo mechi hizo zimepelekwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa ujumla Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea Ijumaa, wenyeji Ndanda FC wakiwakaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi nyingine za Jumamosi, Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
Mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ikumbukwe baada ya mechi 10 za awali, Simba SC wapo kileleni kwa pointi zao 22, sawa na Azam FC wanaokaa nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao, wakati mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 20 ni wa tatu.

0 comments:

Post a Comment