Mrisho Ngasa, anatuachia jina katika zama zake
Katika historia ya kandanda nchini Tanzania majina mengi ya wachezaji wa miaka mbalimbali yamekua yakitajwa, kwa wale waliwashuhudia wachezaji wa miaka ya 1930, 1940 na 1960 watawasimulia wachezaji waliotamba miaka hiyo, na watu wa miaka ya 1970, 1980 & 1990 watawasimulia wachezaji waliotamba kwa miaka hiyo pia, kizazi cha sasa cha miaka ya 2000 kimepata historia kubwa ya wachezaji ambao walifanya vizuri miaka ya 1930-1990, miaka hiyo kuna wachezaji ambao walicheza mpira katika kiwango cha juu sana. Walicheza mpira katika madaraja tofauti lakini sio wote wanaotajwa, wapo wachache sana ambao hutajwa.
Nchi kama Uingereza katika miaka ya 1970,1980 na 1990 yapo majina ambayo yalivuma sana na kuacha historia kama vile Kevin Keegan, Paul Mariner, Mick Mills, lakini miaka ya 2000 karne ya 21 kuna majina pia yamevuma sana na kuacha historia, majina kama David Beckham, Wayne Rooney, Rio Ferdinand, Steven Gerald, Frank Lampard haya ni miongoni mwa majina ambayo yameng’ara sana miaka ya 2000, lakini wapo wachezaji wengi ambao wamecheza ligi hiyo kwa miaka ya 2000 lakini hawakuacha jina lolote la kufanya watu wawakumbuke, kwa mfano ukisema jina kama Hossam Ghaly, Jamie O’hara, Lee Youngpyo Hakuna atakayejua kwa haraka labda kwa wale wadau wa kubwa wa soka, ambao hufatilia sana lakini leo ukitaja Christiano Ronaldo kila mtu hata asiyefatilia soka kama hajamuona basi amemsikia.
Hapa nikirudi katika soka la Tanzania, kutokana na kuchelewa kwa teknolojia imefanya wapendasoka wengi wa Tanzania wasiwashuhudie wachezaji wa miaka kenda iliyopita, licha ya kutokuwepo hata kwa kumbukumbu za kutosha lakini kuna wachezaji wachache wa miaka iliyopita majina yao yanazungumzwa sana, walipita wengi lakini kuna majina yamekua gumzo sana kama vile Zamoyoni Mogela, Edibily Lunyamila, Leodiger Tenga, Othman Mambosasa, Peter Tino, King Kibaden Mputa, Juma Pondamali, Sunday na Kassim Manara, haya ni baadhi ya majina ambayo huwa yanatajwa katika historia ya soka la Tanzania.
Ni jambo kubwa sana mchezaji kuacha jina lake likizungumziwa wakati ameshamaliza karia yake ya kucheza, huo ni upekee mkubwa ambao unahitaji kujitoa, kuwa na nidhamu nzuri, kuwa na uwezo mkubwa na kutoa mchango mkubwa katika timu yake.
Kwa kizazi cha 2000 au karne ya 21 ni dhambi kubwa kuzungumzia wachezaji waliofanya mambo makubwa bila kumzungumzia MRISHO NGASSA, huyu ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba SC ya Dar es Salaam, Khalfan Ngassa (Babu), Alizaliwa Tar 05/05/ 1989, katika wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Kijana huyu alipata mafanikio makubwa ya soka akiwa anatumikia timu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga), alijiunga na Yanga mwaka 2006 akitokea Kagera Sugar ya Kagera, alikua na uwezo mkubwa wa kufunga alikua ana kasi kubwa akiwa na mpira, alikua msumbufu muda wote, Ngassa huyu ndiye yule ambae aliandikwa katika bango moja kubwa lililoshikwa na mtanzania kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Zambia dhidi ya Taifa Stars katika uwanja wa taifa bango hilo lilisomeka “Who is Samatta we have Ngassa”
Baadhi ya wadau wa soka waliandika hivyo kutokana na mchezaji wa Tanzania na TP Mazembe kipindi hicho Mbwana Samatta kutokuwepo katika mchezo huo. Inahitaji ujasiri mkubwa kusema ivyo lakini Ngassa alithibitisha hiyo kauli kwa kuipatia bao moja la ushindi Tanzania, mpaka dakika ya 90 Taifa stars 1-0 Zambia.
Mrisho Ngassa anakipiga katika timu ya Mbeya City inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara kwa sasa, na tayari muda wake unakaribia kumalizika katika karia ya soka, cha msingi Mrisho Ngassa anaondoka huku anatuachia jina lake, ili vizazi vya badae vikisimuliwa au kusoma wachezaji wa zama zilizopita akiwa anatajwa Sunday Manara, Peter Tino, Zamoyoni Mogela, Kibadeni Mputa basi na yeye awekwe ndani, kuwa na Mrisho Ngassa.
Mrisho Ngassa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza michezo mingi katika timu ya taifa, pia ndiye mchezaji ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji bora wa muda wote, katika timu ya taifa, akiwa amefunga magoli 23. Mrisho Ngassa aliwai kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa mwaka 2009-2010 akiwa Yanga, amekua mfungaji bora wa Ligi ya mabingwa Africa akiwa na goli 6, mwaka 2014, alikuwa mfungaji bora wa CECAFA 2009.
Mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania bara mwaka 2010-11, mwaka 2009 alitakiwa na Westham United ya England kwa ajili ya majaribio, hakubahatika kufuzu. Mwaka 2011 alifanya majaribio kwenye klabu ya SettleSounders inayoshiriki ligi kuu Marekani, alibahatika kupata nafasi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Manchester United.
Mwaka 2010 alijiunga na Azam FC ya jijini Dar es Salaam akitokea Yanga kwa uhamisho wa rekodi kwa wachezaji wa ndani, baada ya hapo akajiunga na Simba kwa mkopo akitokea Azam, mwaka 2013, alijiunga tena na Yanga, baadae akajiunga na Free State ya Africa Kusini, baada ya hapo akajiunga na Fanja ya Oman na kwa sasa anachezea Mbeya City.
Huyu ndiye Mrisho Ngassa, naamini kwa karne ya 21 anaacha jina lake, kizazi kijacho kitakutana na jina Ngassa, kama kizazi cha sasa kilivyopokea jina la akina peter Tino.
0 comments:
Post a Comment