Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa sasa imesimama kwa takribani majuma mawili.
Sababu kubwa ya kusimama kwa ligi
hiyo ni kupisha Kombe la Chalenji la CECAFA – michuano inayoratibiwa na
Baraza la Soka kwa nchi za Afrika Mashariki (CECAFA).
Michuano ya CECAFA itafikia ukomo
Desemba 17, mwaka huu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
limetoa ratiba mara baada ya michuano hiyo.
Desemba 22, 23, 24 na 26, zitakuwa siku za mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Mechi zitakazochezwa katika siku
hizo zitafahamika Desemba 5, mwaka huu ambako imepangwa droo ya timu 64
zitakazocheza Raundi ya Tatu ya ASFC.
Timu 64 maana yake ni kuwa timu 16
za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; timu 24 za Ligi Daraja la Kwanza
na timu 24 ambazo zimefuzu kutoka hatua awali; ya kwanza na pili.
Baada ya michezo hiyo, ratiba ya
Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea tena kwa michezo ya raundi ya 12
itakayofanyika Desemba 29, 30 na 31 kabla ya ligi tena kusimama kupisha
michuano ya Kombe la Mapinduzi.
WATANZANIA HAWA KAZINI CECAFA
Baraza la Mpira wa Miguu la nchi
za Afrika Mashariki, limeteua Watanzania wanne (4), kuendesha michuano
ya kuwania Kombe la Chalenji inayoandaliwa na CECAFA.
Watanzania hao ni Alhaji Ahmed
Mgoyi aliyeteuliwa katika Idara ya Mashindano huko CECAFA wakati
mwingine ni Sunday Kayuni ambaye ameteuliwa katika Idara ya Ufundi.
Mgoyi ameteuliwa kutokana na
uzoefu na uwezo wa wake wa kusimamia mashindano ya kimataifa huku akiwa
na rekodi ya kusimamia vema mashindano hayo yalipofanyika kwa mara ya
mwisho nchini Tanzania mwaka 2015 wakati Kayuni ni Mkufunzi
anayetambuliwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Wengine ambao wameteuliwa kuendesha michuano hiyo ni Waamuzi wawili.
Waamuzi hao ni Elly Sasii
(mwamuzi wa kati) na Soud Lilla (Mwamuzi Msaidizi). Tayari wateuliwa
wote wako Kenya kwa ajili ya michuano hiyo.
0 comments:
Post a Comment