Monday, March 5, 2018

MBELGIJI Paul Put ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Guinea, akichukua nafasi ya Mohamed Kanfory Bangoura.
Uteuzi wa Mbelgiji huo ulitangazwa katika mkutano na Waandishi wa Habari mjini Conakry Ijumaa mchana. 
Nafasi hiyo ilikuwa wazi kufuatia kufukuzwa kwa Bangoura mwezi Januari, baada ya Taifa la Syli kutolewa katika hatua ya makundi tu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2018.
Put, mwenye umri wa miaka 61, anatarajiwa kusaini mkataba wake atakapowasili kutoka Kenya ambako aliiongoza Harambee Stars kutwaa Kombe la CECAFA Challenge katika kipindi chake cha miezi mitatu.
Shirikisjo la Soka la Guinea linakabiliwa na mtihani wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za AFCON ya mwaka 2019 nchini Cameroon. 
Kwa sasa Guinea inaongoza Kundi H lenye timu za Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Ivory Coast na Rwanda.
Mechi ya kwanza ya kocha huyo wa zamani wa Gambia na Burkina Faso, Put itakuwa ni ya kirafiki dhidi ya Mauritania mjini Nouakchott Machi 24, 2018.

0 comments:

Post a Comment