Monday, March 5, 2018

Na Haatim Abdul
Asubuhi ya Mei 22, 1990. Ni katika mji wa Vienna huko Austria. Anaonekana mwanaume mmoja wa makamo akiwa amepiga magoti kwa unyenyekevu mkubwa, pembezoni kabisa mwa kaburi. Macho ya mtu huyu yalikuwa yakitiririka machozi mithili ya mvua za rasha rasha. Machozi hayo yakidondokea sakafu ya ukingo wa kaburi hilo lililopo mbele yake. Huzuni ilioje!

Ziara hii haikuwa ya kawaida. Ni ziara iliyojaa msisimko, msisimko wenye majuto ndani yake. Mtu huyu aliyepiga magoti asubuhi hii kaburini akiwaongoza wenzake si mwingine bali ni Eusebio Da Silva. Ndani ya kaburi hili, mwili wa aliyekuwa kocha wake wa zamani aliyeitwa Bela Guttman umelala ukiwa tayari umeoza. Bela hana kauli tena. Lilikuwa ni ombi la kufutiwa laana iliyoikumbuka klabu ya Benfica kabla ya kesho yake kupambana na Ac Milan katika fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Machozi ya Eusebio kwenye kaburi la Bela Guttman hayakuweza kusaidia lolote. Ni Mei 23,1990 katika dimba la Praterstadion mjini Vienna, ikiwa masaa yasiyozidi 24 tangu kufanyika kwa maombi yale. Benfica wanapoteza fainali yao ya sita katika michuano ya ulaya baada ya kukubali kipigo cha goli 1-0 mbele ya AC Milan.
Mnamo mwaka 1961, Benfica wakiwa chini ya Bela Guttman waliweza kuichapa FC Barcelona katika fainali ya klabu bingwa ulaya. Mwaka uliofuata yaani 1962, Benfica waliweza kuiteketeza kabisa Real Madrid kwa kipigo cha goli 5-3 huku kikibakia moja ya kipigo kikubwa zaidi katika historia ya Real Madrid kufungwa katika fainali na ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa Real Madrid kupoteza katika fainali. Isitoshe Madrid wakati huo walikuwa kwenye ubora mkubwa kwenye michuano hiyo.
Ni mafanikio hayo ya Bela Guttman yaliyomshawishi kuuomba uongozi wa klabu ya Benfica chini ya rais Antonio Carlos Vital, imuongezee mshahara. Pamoja na kuisaidia klabu kuleta mafanikio hayo. Bodi ya klabu hiyo ilipiga chini ombi hilo huku wakionesha wazi kuwa hata akiamua kuondoka basi na aende tu. Guttman kwa hasira aliondoka Benfica huku akitoa maneno makali kuhusu klabu hiyo kwa kusema: “Naondoka Benfica kwa huzuni kubwa ila ndani ya miaka 100, Benfica hawataweza kutwaa taji lolote la ulaya

Pengine yalikuwa maneno ya mzaha na yaliyochukuliwa kimzaha na kupuuzwa. Tangu kauli hiyo itolewe, Benfica hawajawahi kutwaa taji lolote la Ulaya huku wakiwa wamepoteza fainali 8 mpaka hivi leo. Pamoja na Benfica kujaribu kujenga sanamu lake nje ya uwanja wake huku kila shabiki akipata fursa ya kumtazama bado haikusaidia kitu kwani laana ya Bela Guttman ingalipo pale pale .
Imepita miaka 56 sasa na Benfica bado wanalia. Hakuna wa kuwaondolea laana hii zaidi ya Bela Guttman ambaye hawezi kuongea tena na hawezi kuwasikia tena. Ni huzuni ilioje!!!

Nikirudi kwa Simba, mazishi ya aliekuwa kiungo mahiri kabisa wa timu hiyo Patrick Mafisango yalijaa utata mwingi, na tuhuma lukuki hasa kuhusu suala la kutokabidhiwa rambi rambi kwa familia yake. Kuna tuhuma kuwa Simba iligoma kutoa fedha hizo za rambirambi kwa madai fedha hizo zilitumika kulipia gharama za mazishi ya kiungo huyo. Mshangao ulioje!!!
Orly Elenga aliyekuwa akiishi na Mafisango nchini Tanzania alipoteuliwa na kufuatilia fedha hizo alipigwa danadana mpaka hivi leo.
Baada ya kupigwa danadana kwa muda mrefu mtoto wa marehemu Mafisango anayeitwa Crespo Mafisango pamoja yake na Orly Elenga waliweza kutoa kauli ambayo inaweza kuonekana ni mzaha tu. Mzaha uliopuuzwa.
Orly alisema “Nasema kwa kitendo hichi, Simba haitakaa ifanikiwe kwa miaka 20 pengine irekebishe suala la fedha za mafisango na wasipofanya hivyo ipo siku watarudi kaburini walipomuacha” Olry akinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti la tarehe 28/8/2012.

Naam! Imepita miaka sita sasa tangu 2012 ambapo Simba walitwaa ubingwa kwa mara ya mwisho. Na ghafla bin vuu sare na Stand United imeleta matumaini mapya kwa Yanga. Ratiba yao pia sio nyepesi wana michezo na Mtibwa huko Morogoro lakini watasafiri pia kuwafuata Njombe Mji huko Njombe na Lipuli huko Iringa. Mtihani mwengine mkubwa ni dhidi ya Singida United huko mkoani Singida. Ratiba hii inaweza kuwapa presha kubwa Simba kuliko Yanga ambao wanasifika kwa kumaliza ligi vizuri.

Na ni wazi kauli hii kuhusu rambirambi ya Mafisango itazungumziwa tu. Bila shaka kimzaha mzaha hivi hivi kilichotokea kwa Benfica kinaweza kutokea kwa Simba kwa kukaa miaka 20 bila taji la ligi kuu ya Tanzania bara. Ni masikitiko kwetu sote. Ni imani ambayo inapaswa isipuuzwe hata kidogo kwa kweli. Lakini muda utatupa majibu kwa wakati sahihi.

0 comments:

Post a Comment