Friday, June 1, 2018


NAHODHA wa Azam FC, Himid Mao Mkami amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Petrojet ya Ligi Kuu ya Misri.
Himid aliyeubukia timu ya vijana ya Azam FC mwaka 2011, yupo mjini Suez nchini Misri tangu juzi na jana amesaini mkataba kuanza kazi chini ya kocha Hassan Shehata.
Himid ameondoka kwa baraka za uongozi wa klabu ya Azam FC na leo Msemaji wa klabi, Jaffar Idd amesema kuwa msimu ujao hawatakuwa na Nahodha wao huyo.
“Uongozi sisi hatuna kipingamizi, Himid ni mchezaji wetu wa muda mrefu tokea akiwa mdogo kabisa ameshiriki mafanikio mengi ya timu, mara baada ya kuleta maombi hayo sisi tulimkubalia na tunamtakia kila la kheri huko aendako katika maisha yake mapya,” alisema.

Himid Mao Mkami amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Petrojet ya Ligi Kuu ya Misri

Wakati huo huo: Azam FC imesema kwamba kocha mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm atajiunga na klabu baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Azam Sports Federation (ASFC) akiiongoza kwa mara ya mwisho klabu yake ya sasam Singida United.
Pluijm ambaye timu yake, Singida United kesho itamenyana na Mtibwa Sugar katika fainali ya ASFC, anakuja Azam FC kuchukua mikoba ya Mromania Aristica Cioaba, aliyekuwa na kikosi hicho msimu uliopita.
“Kwa sasa tumeamua kumtangaza baada ya kukubaliana naye kila kitu, mambo mengine tutayaweka wazi Jumatatu ijayo, na kingine kuanzia msimu ujao Azam FC itakuwa kampuni ikijulikana Azam FC Company Limited,” alisema.
Azam FC inaamini ya kuwa Pluijm ana uzoefu wa kutosha wa soka la Kimataifa na Tanzania utakaoisaidia timu hiyo, akizifundisha kwa mafanikio Singida United na Yanga aliyeipa mataji ya ligi, FA Cup na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya kutua Yanga, Pluijm aliwahi kuzifunza Ashanti Gold, Medeama na Berekum Chelsea zote za Ghana.

0 comments:

Post a Comment