Na alanus
Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania kumwadhibu Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo kutokana na kuwa na cheo ambacho ni kinyume na katiba ya Yanga.
Akilimali ameibuka na kueleza hayo bada ya Makele kuteuliwa kuwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi Yanga ambayo tayari imeshaanza mchakato kuelekea uchaguzi ambao utajaza nafasi za viongozi walioachia ngazi.
Katibu huyo amesema Makele amekalia wadhifa ambao ni kinyume na katiba ya Yanga ilivyo akieleza kuwa haiwezekani akawa Mwenyekiti wa Matawi ya klabu nchi nzima huku pia akawa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi.
Akilimali ameoneshwa kushangazwa zaidi na uongozi wa Yanga kumpa wadhifa huo Makele kitu ambacho amesema ni kuvunja katiba ambayo klabu inaitumia kwa shughuli mbalimbali kuijenga Yanga.
"Ujue mimi nashangaa sana, huyu Makele hakustahili kuwa na nyadhifa mbili Yanga, haiwezekani akawa Mwenyekiti wa Matawi na vilevile akawa kwenye kitengo cha kamati ya uchaguzi kama Katibu, Yanga wamekosea, amevunja katiba'' alisema.
Aidha, Akilimali amefunguka juu ya suala la Mwenyekiti akisema ni wakati mwafaka wa kumpata mbadala wa Yusuph Manji ambaye ameachia ngazi takribani mwaka mmoja na miezi miwili sasa.
Akilimali amezidi kushangazwa na uongozi Yanga ambao upo madarakani mpaka sasa ukiendelea kusema hautajaza nafasi ya Mwenyekiti kuelekea uchaguzi ujao na badala yake watahusika na Makamu pamoja baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Utendaji.
Uamuzi wa Yanga kueleza wanamtambua Manji kama Mwenyekiti ameeleza ni jambo la kupoteza muda kwani tayari ameshatuma barua katika klabu, TFF na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) juu ya kujizulu nafasi hiyo.
Licha ya kutaka Mwenyekiti mpya achaguliwe, Akilimali ameeleza kwa sasa hawezi kutaja wala kupendekeza jina la nani anapaswa kuchukua nafasi ya Manji kwa hofu ya kuonekana mbaya kwa wadau na wanachama wa klabu hiyo na badala yake atasema hapo baadaye.
"Hakuna haja ya kuendelea na mtu ambaye ameshatangaza kujizulu na sasa ni mwaka na miezi miwili hayupo klabuni, ifikie wakati nafasi yake ijazwe kuliko kuendelea kujiaminisha kuwa atarudi"
"Siwezi kumtaja nani anastahili kuwa mbadala wake kwa sasa maana ninaweza kuonekana mbaya kwa baadhi ya wanachama na wadau wa Yanga, nitafanya hivyo baadaye" alisema.
Wakati Yanga ikiwa katika mchakato wa kufanya uchaguzi, tayari TFF imeshatoa siku 75 kwa ajili ya uchaguzi huo ikiwa ni sawa na kwa watani zao wa jadi Simba ambao nao pia utawala wao uliopo madarakani umeshamaliza muda wake.
0 comments:
Post a Comment