Tuesday, August 14, 2018


MAREFA kutoka nchini Namibia ndiyo watachezesha mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya U.S.M. Alger ya Algeria Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
Hao ni Jackson Pavaza atakayepuliza filimbi akisaidiwa Matheus Kanyanga na David Tauhulupo Shaanika ambao wanatarajiwa kuwasili kuanzia kesho.
Yanga SC itajaribu kusaka ushindi wa kwanza katika mechi zake za Kundi D Jumapili baada ya sare moja na kufungwa mechi tatu za awali.

Matokeo mazuri kwa Yanga hadi sasa ni sare ya 0-0 na Rayon Sport ya Rwanda

Yanga SC Ilianza michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 4-0 na U.S.M. Alger nchini Algeria kabla ya kuja kutoa sare ya 0-0 na Rayon mjini Dar es Salaam na baadaye kwenda kufungwa mfululizo na Gor Mahia, 4-0 nchini Kenya na 3-2 Tanzania.
Mchezo wa Jumapili safu ya ushambuliaji ya Yanga itaongezewa nguvu na mshambuliaji mpya, Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambaye amepatiwa leseni na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kocha Mkongo wa Yanga, Mwinyi Zahera anatarajiwa kuwa kwenye benchi la timu kwa mara ya kwanza tangu aajiriwe miezi miwili iliyopita. 

0 comments:

Post a Comment