Friday, August 17, 2018


BONDIA maarufu nchini, Mada Maugo kesho ataonyeshana kazi na Mmalawi, Charles Misanjo katika pambano la kimataifa la uzito wa Super middle kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba.
Wakati Maugo akionyeshana ubabe na Mmalawi, bondia bingwa wa Dunia wa uzito wa Super feather, Ibrahim Class atazipiga na bondia nyota, Baina Mazola katika pambano lingine lenye ushindani mkali kwa mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini.
Mabondia hao wanne leo wamepima afya na uzito kwenye viwanja vya Las Vegas, Mabibo ambapo mabondia wote walitambiana kila mmoja atashinda.

Ibrahim Class (kulia) na Baina Mazola (kushoto) wakati wa kupima uzito leo

Wakati Maugo aliomba waandaaji, kampuni ya Lady In Red Promotion chini ya Mbunge, Sophia Mwakagenda, tambo zaidi zilitawala kati ya Mazola na Class ambao walizindikizwa na ‘vigoma’ ambavyo kulikuwa na akina dada wakimwaga ‘radhi’ mbele ya mashabiki na maofisa wa ngumi za kulipwa.
Mabondia hao wamepima uzito na afya leo huku kila mmoja akitamba kumchakaza mwenzake katika pambano hilo la raundi 10 litakalopigwa kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.
“Nipo serious, naomba waabdaaji waje na machela ili kumbeba Misanjo, nimefanya mazoezi makali na sitaki mchezo mchezo, najua ataleta upinzani kidogo, lakini nimedhamilia kuweka historia kwa kumchapa mwanzoni tu,” alisema Maugo.
Misanjo naye alijibu mapigo kwa kusema hana sababu ya kupoteza pambano hilo na hasa ukizingatia amesafiri umbali mrefu kuja nchini kupambana.
“Namjua Maugo, hawezi kunitisha na kunishinda, nipo kwa ajili ya kumfundisha ngumi kwani nina uzoefu wa muda mrefu na nimepigana na mabondia tofauti katika mataifa mbalimbali,” alisema Misanjo.
Mwandaaji wa pambano hilo, Sophia Mwakagenda alisema maandalizi yote yamekamilika na milango ya ukumbi wa PTA itakuwa wazi kuanzia saa 8:00 Mchana ambapo msanii maarufu nchini, Juma Nature atatumbuiza kabla ya mapambano.
Mwakagenda alisema kuwa pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo yatawahusisha mabondia wakike, Flora Machela ambaye atapambana na Sarafina Julius katika uzito wa Bantam na  Asha ‘Ngedere atazichapa na Happy Daudi katika pambano la uzito wa Super-lightweight. Mapambano hayo yamepangwa kuwa ya raundi sita.

0 comments:

Post a Comment