Na Saleh
Ally
KUMEKUWA na
mjadala mkuu kuhusiana na taarifa kuwa Nahodha wa Yanga, Nadir Ali Haroub
‘Cannavaro’ alipewa kiroba cha kilo 20 na baadhi ya mashabiki wa
Yanga.
Taarifa hizo
zinaenezwa kila sehemu lakini uongozi ulieleza kwamba ulitoa ngao ya heshima
kwake lakini wako mashabiki waliotoa kitunza maji kwa ajili yake ikiwa ni kama
sehemu ya shukurani.
Wanaoanzisha
mjadala wengi wamekuwa wakizungumzia suala la kudhihaki, wakisisitiza kwamba
Yanga imekuwa na njaa ndiyo maana mambo ni magumu hata Cannavaro amepewa mchele
kiasi cha kilo 20 tu.
Kwa kuwa uongozi
umesisitiza kwamba alipewa ngao kama tuzo ya heshima, tunaweza kuliweka kando
suala la kiroba na kama lingekuwepo, basi tutoe heshima kubwa kwa ambaye aliona
awaache nyumbani kwake na kumjali Cannavaro kwa heshima kubwa ambayo anastahili.
Hii ni sehemu ya upendo.
Ukiachana na
yote, nimeamua kuandika kwa ajili ya kuwakumbusha wapenda soka nchini kuhusiana
na Cannavaro, nahodha wa Yanga wa aina yake na mwanadamu ambaye hakukubalika kwa
muda mwingi lakini akaendelea kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda
wote.
Hakuna aliyewahi
kusema Cannavaro mlevi au mtovu wa nidhamu, wengi walilalama kuhusiana na
uchezaji wake wa kibabe, wakisema anaumiza wenzake. Lakini hawakuwa na takwimu
zinazowalinda wala Cannavaro hakuwa na rekodi mbaya ya kadi nyingi sana za njano
au nyekundu.
Cannavaro
aliendelea kuwa beki bora aliyekabana karibu na kila mshambulizi hatari
uliyemjua. Leo anastaafu akifa na mafanikio makubwa kwa mataji huenda kuliko
aslimia 99 ya wachezaji waliowahi kucheza Ligi Kuu Bara kwa kipindi cha miaka 20
iliyopita.
Makombe ya
ubingwa wa Ligi Kuu Bara anayo nane, ubingwa wa Kombe la Shirikisho, Kombe la
Kagame mara mbili lakini katika kabati lake amehifadhi Ngao za Jamii
nne.
Huyu si mtu wa
mchezomchezo na hakika katika mpira wa hapa nyumbani anastahili kuwa mfano wa
kuigwa na isiwe wa kuigwa kwa mashabiki na watu wa Yanga pekee.
Cannavaro
alikuwa nahodha wa timu ya taifa, nahodha aliyefanya vizuri akijituma na
kujitolea kwa juhudi kubwa hadi alipovurugwa na aliyekuwa kocha wake wakati huo,
Charles Boniface Mkwasa.
Cannavaro
hapaswi kuheshimiwa na Yanga na kudhihakiwa na Simba eti kwa kuwa ni watani.
Cannavaro anastahili heshima ya kitaifa na TFF wanapaswa kukumbuka kumtuza kwa
kuwa amekuwa ni nahodha bora, sahihi na mpiganaji kwa taifa lake.
Msiache
Cannavaro akaondoka mkimdhihaki na maneno ya viroba huku mkijisahaulisha yake
bora kwa zaidi ya miaka 15 katika mpira wa Tanzania akiwa bora kwa kiwango cha
uwanjani, nidhamu na maisha nje ya mpira.
Cannavaro
anatakiwa kuendelea kubaki katika vitabu vyetu kama mtu sahihi. Mtu
atakayetumika kuwakumbusha wanaokua na kuwaamsha kwa kuwaaminisha wale ambao
walikuwa wakiamini haiwezekani ili kutenda na kufanikisha kile kilichoonekana
kisingewezekana.
Kama kutakuwa na
shabiki au mwanachama wa Simba anataka kumdharau Cannavaro, basi ni aina ya watu
waliongia katika mpira hivi karibuni au wale ambao wanaamini kuupenda mpira na
kuufurahia ni kuwa na uwezo wa kuzomea pekee.
Angalia upinzani
wa FC Barcelona na Real Madrid, ni zaidi ya upinzani na uadui. Unaanzia
uwanjani, kimkoa, kijimbo, kisiasa na hata kifamilia. Lakini mara zote uliona
Real Madrid wakisimama na kumpigia makofi ya hedhima Andres Iniesta tena katika
mechi ya El Clasico.
Wanaofanya vile
ni Wahispania, wanaonyesha kuikubali kazi ya Iniesta hasa katika kikosi chao cha
timu ya taifa. Lakini wanataka kuthibitisha kuwa wanamthamini kama mfano bora
katika taifa lao la Hispania.
Kweli Tanzania
hatujafika mbali sana, lakini Cannavaro ana mambo ya kuthaminiwa na kupewa sifa
katika taifa letu na si Yanga pekee. Tafadhali tusimdhihaki kwa kuwa hastahili
hicho.
Nimekuwa
nikitamani siku moja kuona Simba wakimpigia makofi Cannavaro kumpongeza ili
kuonyesha nasi tunabadilika. Lakini Cannavaro naye awashukuru Simba kwa kazi
nzuri ya kumfanya awe imara kwa kuwa changamoto zao zilimfanya yeye azidi kuwa
bora hadi kufikia alipo.
0 comments:
Post a Comment