Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire, ameionya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TPLB) kutoanza kubadili mapema ratiba ya Ligi Kuu Bara ikiwa zimebakia siku chache kuanza.
Kauli ya Bwire imekuja mara baada ya tetesi zilizoelezwa kuwa Yanga wametuma maombi kwenda bodi ya ligi wakiomba mechi dhidi yao iliyopangwa kuchezwa tarehe 28 Agosti isogezwe mbele ili wafanye maandalizi baada ya kucheza mtangange wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers Jumamosi ya Agosti 24.
Akizungumza na SPOTI XTRA, Bwire ameitaka bodi kutoanza kuiharibu ratiba mapema namna hiyo kwani itazidi kuleta taswira mbaya kwenye soka la Tanzania.
Ameeleza kuwa wao hawana tatizo na tarehe kubadilishwa lakini kwa namna moja ama nyingine, haitaleta maana nzuri ratiba inapobadilishwa mapema namna hii.
"Si vizuri kwa Bodi ya Ligi kuanza kubadilisha ratiba mapema namna hii wakati hata bado haijaanza.
"Huu utakuwa ni kama ukakasi kwasababu wanapoanza kufanya mabadiliko mapema kiasi hiki itaweza kuleta matatizo mengine baadaye.
"Hatuna tatizo kusogezwa kwa mechi mbele, lakini nashauri tu kwamba si vema mabadiliko haya yakaanza nyakati kama hizi."
Mbali na ushauri huo, kwa upande mwingine Bwire amesema maandalizi yao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara yanaenda vizuri na tayari wako kambini.
0 comments:
Post a Comment