Saturday, August 24, 2019



WAPINZANI wa Yanga, Township Rollers kutoka Botswana, watatumia kilevi cha pombe kama kishawishi cha kuwavutia mashabiki wao kujitokeza uwanjani kuisapoti timu yao itakapopambana.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana katika mchezo wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, saa 10:00 Jioni.

Mchezo huo wa marudiano, umeonekana kuwa gumzo kutokana na wenyeji kuonyesha kuwa na hofu kuelekea katika pambano hilo. Yanga tangu ilipotua nchini Botswana, Jumanne ya wiki hii, imekuwa ikijifua chini ya ulinzi mkali ili kukwepa hujuma za Rollers.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Rollers, hivi sasa wamebuni mpango wa kuwashawishi mashabiki ili kuhakikisha wanaujaza uwanja huo wa Taifa wakati timu hizo zitakaposhuka uwanjani na kuamua kuweka kiingilio kidogo cha Sh 2,000 huku kile cha juu kikiwa ni Sh 10,000.

Rollers wameahidi kuwa siku ya mchezo huo, uwanjani hapo kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwa ni pamoja na pombe ili kuwavutia mashabiki kujitokeza kwa wingi.

“Katika mchezo huu Jumamosi hii, mbali ya soka la kiwango cha juu na la kuvutia, pia kutakuwa na burudani ya muziki na pombe za ‘kumwaga’ uwanjani,” ilisomeka taarifa ya kuwahamasisha mashabiki iliyotolewa na Rollers. Mshindi wa mchezo huo atajihakikishia kutinga Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo.

0 comments:

Post a Comment