Saturday, October 12, 2019


KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeufungia Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kutokana na kuwa na mapungufu kadhaa yanayounyima sifa za kuendelea kutumika kwa michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu nchini.
Pamoja na Mkwkwani, katika kikao cha Kamati ya TPLB kilichofanyika Oktoba 7, mwaka huu kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo, viwanja vingine vilivyofungiwa ni Jamhuri mjini Morogoro, Namfua mkoani Singida, Kinesi Bull wa Shekilango na Bandari wa Tandika mjini Dar es Salaam. 
Kamati ya TPLB imeziagiza klabu ambazo zinatumia viwanja hivyo kutumia kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi kupisha mechi za kirafiki zinazotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kufanya marekebisho au kuchagua viwanja mbadala vyenye sifa.

Aidha, klabu zimekumbushwa kuzingatia Kanuni ya 14 (2), kwani baadhi yao zinapeleka viwanjani magari yenye kitanda badala ya gari la wagonjwa (ambulance) ambalo ndilo linahitajika kwa mujibu wa kanuni, na si gari lolote tu.
Nao Wasimamizi wa mechi vituoni wanatakiwa kuhakikisha ambulance zinapokuwepo viwanjani kama ilivyoelekezwa kikanuni na kwamba huduma ya ambulance isipokuwepo wazuie mechi kuchezwa.

0 comments:

Post a Comment