Aliyewahi kuwa mchezaji wa Yanga, Ally Mayay Tembele, amewapongeza mabosi wa klabu hiyo kuhamishia mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC, kutoka Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwenda CCM Kirumba, Mwanza.
Mayay ametoa pongezi hizo kufuatia taarifa ya Yanga Ijumaa wiki hii kutolewa na Idara ya Habari ndani ya klabu hiyo kuwa mechi hiyo ya kimataifa haitachezewa Uwanja wa Taifa kama ilivyozoeleka.
Mayay alisema maamuzi hayo yataongeza morali na hamasa kubwa kwa Yanga kujipatia mashabiki wengi, tofauti na na Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa, pindi Yanga wanapocheza katika dimba la Taifa kwa miaka ya hivi karibuni, hamasa ya mashabiki kujitokeza kwa wingi imekuwa ndogo tofauti na watani zao wa jadi Simba wanavyotumia faida ya uwanja huo.
"Ni jambo zuri kwa sababu kuna uwezekano Yanga ikapata mashabiki wengi zaidi tofauti na Uwanja wa Taifa ambao umekuwa haupati watu wengi kwa miaka ya hivi karibuni.
"Uzuri wa kanda ya ziwa ni kuwa idadi ya mashabiki kutoka Shinyanga, Mwanza kwenyewe na hata Mara wanaweza wakasafiri kwenda Kirumba sababu si mbali na eneo la tukio," alisema Mayay.
Aidha, kwa upande mwingine straika wa zamani aliyeng'ara akiwa Yanga, Amis Tambwe, amesema kubadili uwanja si sababu ya kufanya vizuri bali aliyejipanga ndiye anaweza kupata matokeo.
"Kubadili uwanja ni mbinu tu za mchezo, kama haujajipanga vizuri utapoteza na ukijinadaa vema utapata matokeo.
"Kikubwa Yanga wajipange vizuri maana kila timu inataka kushinda, maamuzi ya kubadili uwanja hata kama utajaza watu wengi hayawezi kusaidia kupata ushindi zaidi ya kujiandaa kama timu," alisema Tambwe ambaye kwa sasa anaichezea Fanja FC ya Oman.
0 comments:
Post a Comment