WAKATI
homa ya pambano la watani ikipanda, huko Yanga unaambiwa mabosi wa timu
hiyo, wameweka tofauti zao pembeni na kuungana kwa pamoja kuhakikisha
wanamfunga mtani wao, Simba.
Pambano
hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu hizo mbili
kongwe, limepangwa kupigwa Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Timu
hizo zitakutana kila moja ikiwa na benchi jipya la ufundi, Yanga
wenyewe wataongozwa na Kaimu Kocha Mkuu, Charles Mkwasa aliyechukua
nafasi ya Mkongomani Mwinyi Zahera huku Simba wakiwa na Mbelgiji Sven
Vanderbroeck aliyemrithi Patrick Aussems.
Kwa
mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya
Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, mabosi hao walikuwa tayari kufungwa na
timu yoyote katika ligi lakini siyo watani wao Simba.
Mtoa
taarifa huyo alisema mabosi hao wameweka tofauti zao pembeni huku wale
baadhi ya viongozi waliotofautiana kipindi cha uchaguzi uliomuweka
madarakani mwenyekiti Dk Mshindo Msolla na wale wengine waliokuwepo nje
ya timu wakiwa sawa kuhakikisha Mnyama anakufa Taifa, Jumamosi ijayo.
Mtoa
taarifa huyo aliwataja baadhi ya viongozi hao ni Hussein Ndama, Hussein
Nyika, Seif Magari, Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Samuel Lukumay
na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde ambao
wamejipanga kuhakikisha wanawafunga watani wao.
Aidha,
aliongeza kuwa katika kuhakikisha wanaondoa hofu ya hujuma, viongozi
wamepanga kuwalisha yamini wachezaji wake wote kambini mara baada ya
mchezo wao dhidi ya Biashara ambao utapigwa Uwanja wa Uhuru keshokutwa
Jumatatu.
“Kama
unavyojua hivi karibuni uongozi mpya ulitofautiana na baadhi ya wale wa
zamani katika masuala mbalimbali likiwemo suala la mauzo ya jezi mpya
kabla ya GSM kushinda zabuni ya kuuza jezi.
“Hizo
tofauti zao wameziweka kando kwa hivi sasa wakati wakielekea kwenye
pambano la watani wa jadi na hiyo ni kawaida kutokea wakati tukielekea
kwenye mchezo huo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, hivyo
usishangae.
“Katika
hizi timu kutofautiana kawaida sana, lakini linapokuja suala la pambano
la watani wa jadi, basi watu wanaungana kwa pamoja ili kuhakikisha kila
mmoja anapata ushindi.
“Lakini
kwa Yanga wenyewe wameonekana kuungana wote kwa pamoja ili wapate
ushindi na viongozi wao wamepanga kuwatumia wazee wao katika kuwalisha
yamini wachezaji wake wote mara baada ya kuingia kambini kujiandaa na
pambano hilo kwa hofu ya kusalitiwa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia
hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa: “Mechi ya
watani wa jadi siku zote zinawakutanisha watu kwa kuungana kwa pamoja
ili kuhakikisha wanapata ushindi.
“Lakini
nisingependa kulizungumzia hilo suala wakati tayari tuna mchezo mmoja
kabla ya kukutana na Simba, hivyo akili zetu tumezielekea mchezo na
Biashara United na Tanzania Prisons."
0 comments:
Post a Comment