Thursday, January 2, 2020


Kiungo nyota wa zamani wa timu  ya Yanga ambaye aliondoka kwa misimu miwili na kwenda kwa watani wao wa jadi, Simba SC, Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda, hatimaye amerejea tena Yanga mapema leo Alhamisi, Januari 2, 2020.

Niyonzima ambaye aliichezea Yanga kwa miaka sita (2011-2017) alipoamua kujiunga na Simba alikodumu kwa miaka miwili (2017-2019) na kutimkia AS Kigali Rwanda, amewasili katika Uwanja wa  Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na mashabiki wa Yanga wakiongozwa na mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz,  na wanahabari.

Niyonzima anarejea Yanga zikiwa zimesalia siku mbili kufikia Januari 4, ambapo watani wa jadi, Simba na Yanga, watavaana katika Dimba la Taifa.

“Ukitoka sehemu ukarudi ukiwa mzima, ni jambo la kumshukuru Mungu.  Nipo hapa kwa ajili ya Yanga na si kitu kingine, jambo kubwa ni ushirikiano tu. Nakuja leo Tanzania kuungana na timu yangu (Yanga SC), kurejea nyumbani hiyo ni ishara kuwa nipo tayari kuwafanyia kazi,  kwa hiyo kama kuna makosa yalitokea awali naomba tuyasahau.

“Naomba ushirikiano na upendo kama niliopewa kipindi nakuja kujiunga Yanga kwa mara ya kwanza.  Nipo tayari hata kwa mchezo dhidi ya Simba SC japo sipendi kuongelea sana kwa maana mechi hizi zina mambo mengi sana lakini kikubwa ni kujiandaa kisaikolojia. Narudi nyumbani Yanga,” amesema

0 comments:

Post a Comment