Thursday, May 28, 2020





 Na Alanus
BUDUBURAM ni kambi ya wakimbizi iliyo kilomita 44 Kaskazini mwa jiji kubwa zaidi nchini Ghana. Hii ni kambi maalum iliyoanzishwa mwaka 1990 baada ya machafuko na vita katika nchi jirani ya Liberia.

Machafuko hayo na vita kati ya 1989 hadi 1996 na palipotulia tena, mambo yakacharuka mwaka 1999 hadi 2003 na kambi hiyo ikaongezewa wakimbizi hadi kufikia idadi ya 12,000.

Kambi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na taasisi mbalimbali za kujitolea, ile ya wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR lakini pia raia wa Liberia waliokuwa wakiishi nje ya nchi hiyo au wale wenye uwezo.

Maisha katika kambi ya Buduburam hayajawahi kuwa mazuri ana kutokana na msongamano mkubwa wa watu wanaolazimika kuishi chini ya uangalizi kwa kuwa pia si raia wa Ghana.

Kambi hiyo mara nyingi imekuwa na watoto zaidi ya 500 ambao wamekuwa wakipata elimu yao katika eneo hilo na taasisi ya Miller Elementary School ndio iliyojitolea kutoa elimu bure kwa kuwa wazazi wa watoto hao, hawana kitu.

Maisha ya uhamishoni tena wakiishi kwa kulishwa na mashirika hayo yakiwemo yasiyo ya kiserikali na wanaojitolea. Lakini kambi ya Buduburam sasa imeingia kwenye ramani ya dunia ya mchezo wa soka baada ya kuzalisha nyota mpya wa mchezo wa soka ambaye anaamini kuja kuwa beki bora zaidi wa pembeni duniani.

Huyu ni Alphonso Boyle Davis, beki mpya wa kushoto wa Bayern Munich ambaye pia ana uwezo wa kucheza kama winga au kiungo wa pembeni kushoto. Ana ubora ambao sasa amekuwa gumzo kubwa.
Asili ya Davis ni Liberia lakini sasa ni raia wa Canada, uraia ambao aliupata rasmi mwaka 2017 baada ya maisha ya kuhama kutoka nyumbani Liberia akikimbia vita na wazazi wake hadi maisha ya Ghana kabla ya kupata nafasi ya kwenda Canada.

Si kwamba watu walivutiwa zaidi na historia yake ya kuwa aliyeteseka sana na maisha tokea akiwa mtoto mdogo badala yake ni uwezo mkubwa wa kucheza soka ambao ameuonyesha kwa muda mfupi sana.

Bayern Munich ni kama wanaona wamefanikiwa kupata lulu ya jaha kutokana na muda mfupi ambao Davis amekuwa gumzo baada ya kuanza kuitumikia timu hiyo kongwe na kigogo wa soka la Ujerumani.

Si kazi rahisi kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Bayern Munich, lakini Davis ameipata nafasi hiyo na anaonekana anastahili, hakusubiri kuzoea wala hakuwa na sababu ya kupewa muda badala yake amekuwa akifanya vema kabisa.

Tayari vigogo wengine kama Chelsea, Manchester United na Liverpool wanajilaumu kwa kuwa walikuwa wa kwanza kuona kazi bora kabisa ya Davis akiwa Vancouver Whitecaps. Lakini wakaona wanaweza kumpa muda kabla ya Munich kufanya yao mapema. Kumbuka Vancouver Whitecaps ya Canada, aliwahi kuitumikia Mtanzania, Nizar Khalfan.

Kwa sasa Davis ndiye tegemeo la shavu la kulia la Bayern Munich na David Alaba amelazimika kuhama namba na kucheza katikati na mchezaji gumzo zaidi kati ya wachezaji wapya wa Bayern kwa kuwa ameonyesha uwezo mkubwa wakati wa kushambulia lakini bora katika ulinzi.

Bilas haka kwa maana ya mchezaji wa kushoto kwa maana ya beki wa kushoto au winga, Davis ndiye tegemeo la Bayern ikiwa ni mwaka mmoja tu tokea ajiunge na timu hiyo Kwa kuwa umri wake ni miaka 19, alianza kupelekwa Bayern Munich II, hii ni timu ndogo ya Munich na baada ya mechi 6, waliona anastahili kuungana na wakali wengine kama Roberto Lewandowski, Thomas Muller na wengine.

Wakongwe kadhaa waliowahi kucheza Bayern au timu nyingine za Bundesliga wamekuwa wakimtabiria Davis kuja kuwa mchezaji bora zaidi wa upande wa kushoto kuwahi kutokea licha ya kuwa uhamisho wake ulikuwa ni pauni milioni 13.5 tu.

Hii ni kutokana na anavyoendelea kutoa asisti lakini pia uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao. Amecheza mechi 29, tayari ana mabao matatu lakini ana uwezo mkubwa wa kutoa asisti zinazozaa mabao.

Wakati akizaliwa Novermba 2, 2000 katika kambi ya wakimbizi ya Buduburam hakuna aliyejua atakuwa nyota hii leo sawa na mama yake alivyokimbia vita kwao Liberia akiwa na mimba ya nyota huyo ambaye tayari ameandika rekodi nyingi sana. Kwa sasa inaonekana ndiye mchezaji aliyezaliwa katika miaka ya 2000 mwenye rekodi kubwa na nyingi zaidi katika soka la ushindani, duniani kote.

Baadhi ya rekodi hizo, Machi 17, mwaka huu alifunga bao lake la kwanza akiwa Bayern Munich ambaye alianza kuichezea Januari mwaka huu. Bao hilo aliandika rekodi ya kufunga bao akiwa na umri wa miaka 18, mieizi minne na siku 15, aliyekuwa na rekodi hiyo alikuwa ni Roque Santa Cruz, miaka 20 iliyopita.
Akiwa bado ana miaka 18, aliingia kwenye rekodi ya kuwa katika kikosi cha kwanza cha Bayern Munich kushinda mataji mawili ya Bundesliga na lile la Kombe la Ujerumani.

Wiki chache baadaye akaitumikia kwa mara ya kwanza Bayern Munich inayocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Olimpiakos na asisti yake ya kwanza katika mechi ya michuano hiyo dhidi ya Chelsea, Lewandowski akimalizia kazi.

Mwendo wa Davis ambaye mara kwa mara alikuwa mkimbizi maana wazazi wake walikimbia vita, yeye akazaliwa kambini akiwa mkimbizi unaonyesha au lazima utafikia katika mafanikio na hakuna wa kuuzuia.

Kuna wakati baba yake aliwahi kusema kuwa mara kadhaa wakiwa sebureni wakiangalia mpira, alikuwa akimuambia baba siku moja utaniona hapa nikicheza, jambo ambalo kweli limetokea na anaamini mengi ambayo ameyatamka na ambayo hajayasema, ataweza kufanya yatokee.

0 comments:

Post a Comment