Pondamali ambaye ni mlinda mlango wa zamani wa klabu hiyo kongwe nchini, alitimuliwa mwaka jana baada ya klabu hiyo kuvunja benchi lote la ufundi lililokuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera.
Kocha huyo anayeinoa African Sports kwa sasa, amesema kuwa baada ya kuona hakuna dalili za kulipwa madeni yake, ameamua kupeleka suala hilo TFF anakoamini atapata haki yake.
“Wakati tunaondolewa nilikuwa nikidai mshahara wa miezi saba, uongozi ulisema utanilipa ndani ya muda mfupi lakini imekuwa tofauti na makubaliano,” amesema Pondamali.
Amesema kabla ya uchaguzi mkuu wa mwisho kufanyika kwenye klabu ya Young Africans walifanya kazi katika mazingira magumu ikiwamo kutolipwa mshahara kwa miezi hiyo saba.
“Klabu ilikuwa kwenye hali ngumu na tulifanya kazi kwa mazingira hayo hayo, tukiamini uongozi mpya ukiingia madarakani utatulipa, lakini ikawa tofauti, tukaishia kuondolewa.
“Tuliambiwa baada ya siku chache tutalipwa fedha zetu, lakini imekuwa ndivyo sivyo na binafsi nimeona sina njia nyingine ya kupata haki yangu zaidi ya kwenda kushtaki TFF,” anasema.
Mwenyekiti wa Young Africans, Dk Mshindo Msolla alikiri klabu hiyo kudaiwa.
“Si Pondamali pekee ambaye anatudai, klabu inadaiwa na watu mbalimbali na madeni yote tunayatambua na tutayalipa,” anasema Dk Msolla.
0 comments:
Post a Comment