KLABU ya Yanga imeibua upya utata mwingine wa mkataba wa mshambuliaji Bernard Morrison wakidai hana mkataba halali na mabosi wake wa sasa ambao ni Simba.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela amesema hayo leo Oktoba Mosi kwa kueleza kuwa wakati klabu yao ikipokonywa haki ya umiliki wa Morrison wamebaini mapungufu makubwa katika mkataba wa mchezaji huyo na Simba.
Mwakalebela ambaye amekuja na nakala anayodai ni ya mkataba huo amesema sehemu zote za mkataba huo zimesainiwa na mchezaji huyo pekee hatua ambayo sio sahihi.
Amesema katika mkataba huo pia hauna sehemu iliyosainiwa na kiongozi yoyote wa bodi ya Simba lakini pia hauna saini ya shahidi.
Pia,amesema katika kila nakala imesainiwa na Morrison pekee bila ya upande wa pili hatua ambayo inaoonyesha watani wao hao hawakuridhia mkataba huo.
“Una mapungufu makubwa katika sehemu mbili…hakuwa na shahidi lakini amesaini kwenye upande wake, CEO wa Simba hajasaini. Simba SC haijaridhia mkataba wa Morrison kwa sababu hakuna sehemu yoyote ambapo klabu ya Simba imesaini mkataba wa Morrison.
"FIFA inamtambua Morrison ni mchezaji wa Yanga. TMS ya FIFA inamtambua Morrison mchezaji wa Yanga. Mkabata wa Simba na Morrison una dosari, upande wa mchezaji umesainiwa bila shahidi,” amesema Makamu Mwenyekiti Yanga, Fredrick Mwakalebela.
Usajili wa Morrison kutoka Yanga kuibukia Simba umekuwa na sarakasi nyingi tangu awali ambapo mwanzo kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya mchezaji na mabosi wake wa Yanga.
Yanga walikuwa wakieleza kuwa mchezaji huyo ana dili la miaka miwili huku mchezaji akieleza kuwa ana mkataba wa miezi sita na umemalizika.
Utata huo ulifanya suala hilo kutinga makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo kesi yake iliskilizwa kwa muda wa siku tatu mfululizo na hukumu ilitolewa kwamba Morrison ni mchezaji huru kwa kuwa mkataba wake na Yanga ulikuwa na mapungufu.
Kwa sasa limeibuka tena sakata hili ambalo nalo linaeleza kuwa bado Morrison mkataba wake ndani ya Simba una mapungufu muda ambao dirisha la usajili limefungwa na mchezaji huyo akiwa ameshacheza mechi ndani ya Simba.
0 comments:
Post a Comment