Mchezaji nyota wa zamani wa kandanda Diego Maradona amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60.
Kiungo huyo mshambuliaji wa Argentina awali mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa ubongo ambao madaktari walimwambia ulifaulu.
Baada ya upasuaji huo, ilitangazwa kuwa Maradona angeanza matibabu ya uraibu wa pombe.
Maradona ni moja ya wachezaji bora zaidi wa kandanda kuwahi kutokea.
Mwaka 1986 akiwa nahodha wa Argentina, aliliongoza Taifa lake kushinda Kombe la Dunia nchini Mexico huku akionesha uwezo binafsi mkubwa katika ushindi huo.
Alizichezea klabu za Barcelona ya Uhispania na Napoli ya Italia. Akiwa na Napoli alinyakua ubingwa wa ligi ya Serie A kwa misimu miwili.
Maradona aliifungia Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia.
Aliliongoza Taifa lake katika fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 1990 nchini Italia, ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi.
Alikuwa tena nahodha wa taifa lake katika mashindano ya 1994 nchini Marekani lakini alirudishwa nyumbani baada ya kubainika alitumia dawa za kuongeza nguvu.
Katika miaka yake ya mwisho ya uchezaji aligubikwa na utumiaji wa dawa za kusisimua misuli pamoja na dawa za kulevya.
Maradona alitaabika na matumizi na uraibu wa dawa za kulevya aina ya cocaine na alifungiwa kucheza mpira kwa miezi 15 baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia dawa hizo mwaka 1991.
Alistaafu kusakata kandanda la kulipwa mwaka 1997 katika siku ya kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwake, akiwa na klabu maarufu nchini Argentina ya Boca Juniors.
Maradona alichaguliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Argentina mwaka 2008 na akaachana na kibarua hicho baada ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambapo Argentina ilitolewa na Ujerumani katika hatua ya robo fainali.
Baada ya hapo akaenda kuvinoa vilabu kadhaa katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na kisha Mexico.
Mpaka umauti unamfika alikuwa na timu ya Gimnasia y Esgrima inayoshiriki ligi kuu ya Argentina.
Ulimwengu wa soka wamlilia
Nyota wa zamani wa Brazil Pele ameongoza salamu za rambirambi kwa msiba wa Maradona, akitoa taarifa fupi akisema: "Siku moja tutacheza pamoja mpira juu mawinguni."
Mshambuliaji nyota wa zamani wa England Gary Lineker amesema: "Mchezaji bora zaidi wa toka langu na yawezekana. mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea. Baada ya maisha ya baraka na mikasa, natumai atapata utulivu katika mikono ya Mungu."
0 comments:
Post a Comment